Ghasia zaendelea Mombasa kwa siku ya pili baada ya mauaji ya Rogo

Agosti 28, 2012

  • 4 Maoni
  • Chapisha
  • Panga upya Punguza Ongeza

Waandamanaji walipambana na polisi katika mji wa bandari ya Kenya, Mombasa, kwa siku ya pili hapo Jumanne (tarehe 28 Agosti) baada ya mauaji ya Aboud Rogo Mohammed , mhubiri wa Kiislamu wa Kenya aliyefungamanishwa na al-Shabaab, liliripoti shirika la habari la AFP.

Wafanyakazi katika hospitali kuu ya Mombasa waliripoti kwamba kiasi ya watu 14 walijeruhiwa katika mapambano hayo, wakiwamo askari wawili wa kutuliza ghasia.

Mamia ya vijana wenye hasira waliyashambulia makanisa, kurusha mawe, kuharibu magari, kuzishambulia biashara na kupiga mayowe ya kumuunga mkono Rogo huku polisi wakijaribu kuwadhibiti.

"Tunajaribu kuwadhibiti ili tusisababishe vifo zaidi. Vifo na uharibifu wa mali hautasaidia chochote," alisema mkuu wa polisi wa mkoa huo, Aggrey Adoli.

Polisi wa Kenya walitumia mabomu ya machozi na kurusha risasi za mpira kuwazuia waandamanaji na kuwakamata watu 12 siku ya Jumanne, liliripoti gazeti la Daily Nation la Kenya.

Baraza Kuu la Waislamu la Kenya (SUPKEM) na jumuiya kadhaa za Kiislamu zimelaani ghasia hizo, hasa kuyalenga makanisa, ambapo matano kati yao yamechomwa moto.

"Ghasia kama hizi ni kinyume na imani yetu. Waandamanaji wasijifiche nyuma ya Uislamu au aina yoyote ya mafunzo yake," alisema Katibu Mkuu wa SUPKEM Adan Wachu, kwa mujibu wa AFP. "Hawa ni wahalifu na wachukuliwe hivyo."

Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, alilaani mauaji dhidi ya Rogo, akiongeza kwamba serikali "imejitolea kuwafikisha wahusika mbele ya sheria."

Rogo alikuwa "kiongozi mkuu wa kiitikadi" wa kundi la Hijra nchini Kenya, ambalo pia hujulikana kama Kituo cha Vijana wa Kiislamu (MYC), kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. MYC inaonekana kama mshirika wa karibu wa al-Shabaab nchini Kenya .

Kutokana na mauaji hayo, al-Shabaab iliwatolea wito Waislamu wa Kenya "kuchukuwa hatua zote muhimu" kuilinda dini yao.

"Waislamu wanapaswa kulichukulia jambo hili mikononi mwao, waungane dhidi ya makafiri na kuchukua hatua zote muhimu kuilinda dini yao, heshima yao, mali zao na maisha yao dhidi ya maadui wa Uislamu," ilisema taarifa ya al-Shabaab.

Unaonaje kuhusu makala hii? (Jumla ya Kura 9)

Dislike_icon(5)

(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji

Maoni ya msomaji

  • Catrina fire
    August 30, 2012 @ 04:54:15AM

    vitendo kama hivyo serikali inapaswa kuwatia vijana wote mbaroni watakao patikana wakishirili katika visa hivyo kwene wengi wao ni wale hawana kazi zakufanya.

  • Lohay Langay wa Gallapo
    August 29, 2012 @ 05:41:08AM

    Daima huwa ninashangaa sana pale, anauawa mtu moja alafu makanisa, mabaa yanashamuliwa, hapo ninapata wasiwasi kuwa bado hatuna umoja kama waafrica. Bali tunakuwa watu wa kuongozwa na matukio

  • ares
    August 29, 2012 @ 04:43:12AM

    Ni pahali pazuri pa kujifunza masuala ya kikanda.

  • william wangome kimani
    August 29, 2012 @ 01:49:17AM

    Nimehamaki sana. Ama vijana hawa wa Kiislamu wanaamini kwamba wengine sio vijana kwa sababu tu wao sio Waislamu au hawapati mafundisho sahihi popote pale wanapopata darasa za Kiislamu. Hatuko vitani nao na ninasema kwa ufupi tu watoke Kenya waende kufanya vita huko ambako wanaishi kwa kumwaga damu. Hasira kwa walengwa wasiohusika ni hasara kubwa kwa watu wasio na hatia.

Habari Mpya kabisa

Katika Mwangaza

Jisajili

Kura

Je, unadhania kupigwa marufuku kwa hotuba ya chuki na Tanzania kutakomesha mashambulizi dhidi ya makanisa na misikiti?

Angalia matokeo