Juni 25, 2012
Baada ya siku tatu za mazungumzo wiki iliyopita katika mji mku wa Kenya, Nairobi, viongozi wa Somalia walifikia hatua za mwisho za rasimu ya katiba na kukubaliana katika vifungu kadhaa kwa ajili ya kumalizika kipindi cha mpito cha serikali ya Somalia.
Mikutano ilifanyika kuelezea masuala ambayo bado hayajatatuliwa na kukamilisha makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni katika mkutano wa mwezi Mei mjini Addis Ababa kuhusiana na utekelezaji wa mpango wa amani kumaliza kipindi cha mpito kufikia tarehe 20 Agosti.
Waziri Mkuu wa Somalia, Abdiweli Mohamed Ali, alisema kukubaliwa kwa katiba kulikuwa jukumu muhimu la kumaliza kipindi cha mpito na aliwataka viongozi wengine kuendelea na kuchukua hatua za kufikia mwisho huo.
“Mabibi na mabwana, tuna siku 58 za kuandika historia. Tusipoteze hata dakika moja,” alisema katika hotuba ya kufunga mkutano huo wa Nairobi hapo Ijumaa (tarehe 22 Juni).
Mkutano huo ulifanywa chini ya uwezeshaji wa Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia, Balozi Augustine Mahiga, ambaye pia aliyasifu makubaliano ya viongozi hao kama hatua muhimu katika kipindi cha mpito cha utawala wa serikali ya shirikisho.
“Hatua hii ya Nairobi ni hatua kubwa kabisa kwa sababu inashuhudia kukamilika kwa moja ya hatua kubwa za kumaliza kipindi cha mpito,” alisema.
“Nimefurahishwa sana kwamba wadhamini wote wamekusanyika pamoja katika moyo wa ushirikiano na muafaka na wamejitolea kabisa kupiga hatua mbele,” alisema Mahiga. “Kipindi cha mpito kitakamilika chini ya siku 60 zijazo na hatuna wakati wa kupoteza.”
Waziri Mkuu, Rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, Spika wa Bunge Sharif Hassan Sheikh Aadan, Rais wa Puntland Abdirahman Mohamud Farole, Rais wa Galmudug Ahmed Mohamed Alin na mwakilishi wa Ahlu Sunna wal Jamaa, Khalif Abdiqadir Maalim Nur, walihudhuria mkutano huo wa Nairobi.
Kamati chini ya uongozi wa Waziri wa Masuala ya Katiba na Maridhiano, Abdurahman Hosh Jibril, itawasilisha rasimu ya katiba kwa Bunge la Katiba hapo tarehe 12 Julai. Hii inaipeleka mbele ile tarehe ya mwisho iliyokuwa imewekwa na viongozi wa Somalia mjini Addis Ababa ya tarehe 2 Julai.
Bunge la Katiba litakuwa na muda wa hadi tarehe 20 Julai kujadili na kuipigia kura katiba hiyo, ambapo baadaye itapelekwa kwa raia wa Somalia kuthibitishwa kwa kura ya moja kwa moja ya maoni.
Wadhamini wa mpango wa amani walithibitisha kwamba bunge jipya la Somalia litakuwa na wajumbe 225, hata kama viongozi wengine wa kikabila walitaka liwe na wajumbe 275.
Viongozi wa Somalia walirejea ahadi yao ya kuunda kamati kadhaa kumaliza kipindi cha mpito, ikiwemo jopo la viongozi wa makabila na kamati ya ufundi kuwasaidia viongozi hao wa makabila kutatua migogoro, na ofisi ya uratibu itakayofuatilia mawasiliano baina ya washiriki katika kipindi cha mpito.
Wachambuzi wa mambo ya siasa wa Somalia walieleza imani yao kwa uwezo wa viongozi kutekeleza ahadi zao za kukamilisha muda wa serikali ya mpito kufikia tarehe 20 Agosti na kuvishinda vikwazo vyovyote vya kiutendaji au migogoro ya kimaslahi inayoweza kujitokeza katika kipindi kilichobakia.
Abdirashid Abdullahi, mchambuzi wa masuala ya siasa na profesa wa chuo kikuu, alisema makubaliano ya Nairobi ni alama ya utiifu wa viongozi kwa ahadi yao waliyoitoa kumaliza kipindi cha mpito.
“Somalia sasa iko kwenye hatua ya kufanya maamuzi kwenye historia yake na viongozi wake wa kisiasa lazima wawe wakweli kwa ahadi waliyoiweka kumaliza kipindi cha mpito kwa sababu ukamilishaji huo unawakilisha matakwa ya watu wa Somalia,” aliiambia Sabahi.
Abdullahi alisema watu wa Somalia wanatarajia enzi mpya ya matumaini na utulivu itawasili ndani ya mwezi Agosti.
“Viongozi wa kisiasa wasiitupe fursa hii,” alisema. “Pia, viongozi wa makabila wanaokutana Mogadishu wasicheleweshwe mchakato wa kuwachagua wajumbe wa Bunge la Katiba, lenye jukumu la kupitisha katiba mpya, ikifuatiwa na kuchaguliwa kwa wajumbe wapya wa bunge, linaloweza kusafisha njia kwa kumalizika kipindi cha mpito kwa wakati.”
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Farah Mohamed Yusuf, alisema kumalizia rasimu ya katiba mpya kunachukuliwa kama jukumu muhimu kabisa la kukamilisha kipindi cha mpito.
“Uthibitisho wa viongozi wa Kisomali kwamba wamejitolea kukamilisha mchakato huu na imani yao ya pamoja kukamilisha kipindi cha mpito ni hatua muhimu sana ambayo itafungua enzi mpya kwa mustakabali wa Somalia,” aliiambia Sabahi.
Baada ya miongo ya vita, uchafuzi na machafuko, Somalia sasa inaelekea kwenye amani na muafaka wa kitaifa na kufikia mwisho wa kipindi cha mpito,” alisema Yusuf.
Polisi nchini Tanzania walimkamata mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msingwa, na wafanyabiashara 60 k...
Mahakama moja ya Bosaso iliwatia hatiani na kuwapiga faini Wairani 78 siku ya Jumapili (tarehe 19...
Polisi nchini Tanzania waliwakamata watuhumiwa 15 kuhusiana na kulichoma Kanisa la Bethania kweny...
Mkuu wa Polisi wa Kenya, David Kimaiyo, ameondoa nafasi za afisa polisi wa jimbo, afisa wa upelel...
Watu wenye silaha waliwaua watu wawili na kuwajeruhi wengine wanne katika mashambulizi tofauti kw...
Mkutano wa kuzungumzia uwezekano wa uchimbaji mafuta na gesi, uwekezaji, usalama na miundombinu n...
Wizara ya Masuala ya Wanawake na Familia ya Puntland ilianza mafunzo ya siku nane hapo Juampili (...
Zaidi ya Wasomali milioni 1 hawatakuwa na "usalama wa chakula" hadi mwezi wa Septemba, Mtandao wa...
Ujumbe kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Pembe ya Afrika (IGAD) uliwatembelea maafisa mjini Mogadish...
Mshukiwa wa ugaidi na mke wake walipigwa risasi na kufa na maafisa sita wa polisi walijeruhiwa wa...
(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji