Juni 20, 2012
Baadhi ya wabunge wameelezea kutokuridhika kwao na bajeti ya taifa iliyowasilishwa bungeni na serikali hapo tarehe 14 Juni, wakisema imekosa uwekezaji kwenye kupambana na umasikini na kuiendeleza nchi.
Waziri wa Fedha William Mgimwa alitangaza kwamba serikali inapanga kutumia shilingi trilioni 15.1 (dola za Kimarekani bilioni 9.5) kwa mwaka ujao wa kifedha, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12 kutoka ile ya mwaka uliopita. Matumizi ya uendeshaji yatagharimu shilingi trilioni 10.6 (dola bilioni 6.7), huku shilingi trilioni 4.5 (dola bilioni 2.8) zikitengwa kwa miradi ya maendeleo.
Wakosoaji wanasema serikali inapaswa kuipitia bajeti kwa sababu inaongeza deni la taifa na kukata kwenye maeneo muhimu kama maendeleo, miundombinu na elimu.
Luhanga Mpina, mbunge kutoka chama kinachotawa cha Mapinduzi (CCM), alisema alitarajia bajeti hiyo kutenga fedha zaidi kwa maendeleo ya kilimo, elimu ya juu na miundombinu kama vile reli, viwanja vya ndege na barabara.
“Serikali inakosa umakini katika masuala muhimu. Bajeti nzima imejikita kwenye malipo kwa semina, usafiri na masuala ya kifahari, lakini sio kwa maendeleo. Vipi wanaweza kutenga asilimia 30 tu kwa maendeleo na asilimia 70 kwa matumizi ya ueshaji?”, alisema Mpina. Aliiambia Sabahi kuwa bajeti ya maendeleo lazima iwe hadi asilimia 35 ya bajeti yote. Mwaka jana ilikuwa asilimia 37.
Wabunge walianza rasmi kuijadili bajeti hiyo hapo Jumatatu (tarehe 18 Juni) na wanatarajiwa kuipigia kura mwishoni mwa wiki hii. Ikiwa bajeti hiyo itapingwa kwa ujumla wake, katiba inaagiza kuvunjwa kwa bunge na kuitisha uchaguzi mpya.
Mbunge wa CCM, Alphaxard Lugola, alisema nchi haiwezi kuendelea bila kuwa na uwekezaji katika umeme, usafiri wa reli, kilimo, huduma za maji na afya.
“Tunahitaji kuwekeza sana kwenye reli. Kila sehemu duniani – nenda Ulaya, Marekani na Asia – sheheha kwa shehena husafirishwa kwa njia ya reli,” Longola aliiambia Sabahi.
Mgimwa alisema serikali haikuyakana maendeleo kwenye bajeti, bali imejikita zaidi katika changamoto zinazoukabili uchumi, ukiwemo ukuaji wa uchumi, usalama wa chakula na kupanda kwa gharama ya maisha.
Alisema serikali imetenga shilingi bilioni 192 (dola milioni 122) kwa mpango wa Kilimo Kwanza wa kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na cha kibiashara na kukuza kujitegemeza.
Serikali pia inapanga kuendeleza sekta za nishati, ujenzi, uchimbaji madini, utengenezaji wa bidhaa na teknolojia ya habari ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kuinua uchumi, alisema Mgimwa, akiongeza kwamba serikali inapanga kuimarisha mazingira ya kibiashara kuhamasisha wajasiriamali wadogo wadogo.
“Hili litatusaidia kutengeneza nafasi za ajira -- hasa kwa vijana -- kuwekeza katika miundombinu ya nishati, hasa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, barabara, bandari, na reli ili kupunguza gharama za kufanya biashara na kuongeza uzalishaji,” Mgimwa aliliambia bunge, akiongeza kwamba kuongeza uzalishaji kutasaidia kulipia deni la nchi.
Mgimwa alisema deni la taifa linalipika na kwamba miradi ya miundombinu inahusika na sehemu kubwa ya fedha zilizokopeshwa.
“Kwa kuzingatia nafasi yake kwenye maendeleo ya miundombinu muhimu, serikali inaendelea kutafuta mikopo ya ndani na nje kwa kufadhili miradi ya maendeleo,” alisema. “Matokeo yake, hadi Machi 2012, deni la nje na ndani lilifikia shilingi trilioni 20.3 (dola bilioni 12.8)” – likiwa ni kubwa zaidi kwa asilimia 15 na lile la mwaka jana na mara mbili zaidi ya shilingi trilioni 11 (dola bilioni 7) ya ilivyokuwa mwaka 2009.
Zitto Kabwe, mbunge kutoka chama cha upinzani cha CHADEMA, alisema deni la taifa limekua kwa kiwango kinachotisha na lazima kipunguzwe.
“Wamezifanya nini fedha? Nani aliamuru ukopaji huu mkubwa? Sipingi kuchukua mikopo, lakini wamezifanya nini pesa zote hizi? Serikali inapaswa kutoa maelezo,” Kabwe aliiambia Sabahi.
Mgimwa alisema serikali haikusudii kulishinikiza bunge, lakini inawakumbusha wabunge kwamba wana jukumu muhimu mbele yao – ambalo linaweza kutatuliwa kwa ushirikiano.
“Tatizo letu ni pesa,” aliiambia Sabahi. “Tuna mipango tuliyoiweka kwa karibuni kila kitu wanachosema, lakini uwezo wa kuifadhili ni tatizo. Ninafurahi baadhi ya wabunge wanapendekeza kutanua eneo la kodi…Kwa pamoja tunapaswa kutafuta suluhisho, na sio kubebesha lama tu.”
Baadhi ya wabunge wa Somalia wameitupilia mbali hoja ya kumtaka waziri mkuu na baraza lake la maw...
Wabunge wa upinzani walidai kwamba serikali ya Tanzania imekuwa ikibana uhuru wa kujieleza na kud...
Sampuli ya DNA iliyochukuliwa kwenye mswaki uliokuwemo kwenye begi lililokuwa na risasi lililopat...
Wakenya kumi na wasaba wameshtakiwa kwa kuvunja amani, kufanya ghasia na ukatili dhidi ya wanyama...
Al-Shabaab imedai kuhusika na urushwaji wa makombora kwenye kasri ya rais mjini Mogadishu siku ya...
Wanajeshi wa Uganda wa Kikosi Namba 9+ wanarudi nyumbani baada ya kukamilisha miezi 13 ya ziara y...
Kikosi cha polisi cha Kenya kitaanza uhakiki wa kina wa maofisa mwezi ujao, kikianza na kusaili w...
Ujambazi ulizuiwa katika ofisi za usalama za Wells Fargo huko Mombasa ulisababisha kifo cha watu ...
Rais wa Ghana John Dramani Mahama aliahidi msaada wa nchi yake katika kipindi cha ujenzi mpya wa ...
Polisi nchini Tanzania walimkamata mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msingwa, na wafanyabiashara 60 k...
(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji