Somaliland yakaribisha ufunguzi wa kiwanda kipya cha vinywaji

Na Barkhad Dahir, Hargeisa

Mei 31, 2012

  • 2 Maoni
  • Chapisha
  • Panga upya Punguza Ongeza

Kiwanda kipya cha vinywaji baridi kilichofunguliwa karibu na Hargeisa wiki iliyopita kitasaidia kuinua maendeleo ya kiuchumi na kupunguza kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira katika eneo hilo, wanasema wachambuzi.

  • Rais wa Somaliland, Ahmed Mohamed Silanyo (katikati) wakati wa ufunguzi wa kiwanda kipya cha vinywaji baridi mjini Hargeisa. [Barkhad Dahir/Sabahi]

    Rais wa Somaliland, Ahmed Mohamed Silanyo (katikati) wakati wa ufunguzi wa kiwanda kipya cha vinywaji baridi mjini Hargeisa. [Barkhad Dahir/Sabahi]

  • Rais Silanyo na maafisa kutoka SBI na Coca-Cola wakitembelea kiwanda cha vinywaji huko Hargeisa. [Barkhad Dahir/Sabahi]

    Rais Silanyo na maafisa kutoka SBI na Coca-Cola wakitembelea kiwanda cha vinywaji huko Hargeisa. [Barkhad Dahir/Sabahi]

Kwa kushirikiana na Coca-Cola, Tasnia ya Vinywaji ya Somaliland (SBI) imejenga kiwanda hicho katika mji wa Jalelo, umbali wa kilomita 30 kaskazini mashariki mwa Hargeisa.

Rais Ahmed Mohamed Silanyo wa Somaliland, Rais wa Kitengo cha Biashara cha Coca-Cola kwa Afrika Mashariki, Kati na Magharibi, Nathan Kalumbu, Afisa Mtendaji Mkuu wa SBI, Ahmed Osman Gelleh, pamoja na maafisa wengine wa serikali walihudhuria sherehe za ufunguzi wa kiwanda hicho hapo tarehe 22 Mei.

Kampuni hizo mbili zimewekeza dola milioni 15 katika mradi huo, alismea Kalumbu wakati wa sherehe. Mradi huo ni sehemu ya dhamira wa Coca-Cola kuwekeza dola bilioni 12 barani Afrika kufikia mwaka 2020, mpango ulioanza mwaka 2010, alisema.

Utengenezaji wa nafasi za kazi na maendeleo ya kiuchumi

Kiwanda hicho kipya ni hatua iliyo kwenye muelekeo sahihi na jambo ambalo litaisadia Somaliland kupata maendeleo zaidi, alisema Silanyo katika hotuba yake.

“Ninapenda kuwapongeza Coca-Cola na SBI; wanafanya kitu ambacho tunaweza kujivunia. Ufunguzi wa kiwanda hiki utawasaidia watu kujifunza stadi mpya, utaisaidia Somaliland kujitangaza duniani [kwa uwekezaji wa kimataifa] na kutengeneza nafasi mpya za ajira,” alisema.

Meneja Mkuu wa Operesheni wa SBI, Mustafe Osman Gelleh, alielezea matumaini na imani yake kwamba kitega uchumi hicho kitatengeneza nafasi za ajira kwa Wasomali. Alisema kiwanda hicho kwa sasa kimewaajiri watu 200 na kinakisia kwamba itasaidia na kuunga mkono nafasi nyingine 6,000 za ajira zisizo za moja kwa moja kupitia sekta uuzaji wa rejareja na usambazaji.

Alisema nchi hiyo ilikuwa haina wafanyakazi wenye ustadi na kampuni ililazimika kutumia wafanyakazi kutoka nje kwa muda kuanza kazi ya uzalishaji na kusaidia kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wapya.

“Hakuna wetu wengi wenye ujuzi unaohitajika kwa kazi ya uzalishaji kiwandani, hiyo ndiyo sababu mwanzoni tulileta wafanyakazi kutoka nje. Hivi sasa tumewafundisha wafanyakazi wa ndani ambao wamechukua baadhi ya kazi,” Mustafe aliiambia Sabahi.

Kiwanda hicho kilichojengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 10,000 kitaweza kutoa kreti 18,000 kwa siku, alisema. Uzalishaji unatarajiwa kusambazwa katika maeneo ya Somaliland, Puntland, Galmudug na baadhi ya masoko ndani ya Somalia, alisema.

"Tunapenda kuwashukuru watu wa Somaliland na kuwataka wafanye kazi nasi na kutuunga mkono ili tuhamasishe uzalishaji wa ndani wa bidhaa,” alisema meneja wa operesheni wa SBI.

Kuwekeza wa siku za baadaye

Waziri wa Biashara na Utalii wa Somaliland, Abdirisak Khalif Ahmed, alisema programu za mafunzo zitatengeneza nafasi zaidi za ajira, wakati huo huo kuwapa ujuzi watu wanaotafuta ajira, ambao wanaweza kuutumia hapo baadaye.

Alisema kwamba sio tu kiwanda hicho cha vinywaji baridi kinatengeneza nafasi za ajira bali pia kusaidia kuvutia uwekezaji mwengine wa kigeni.

Ahmed alisema wawekezaji wa Somaliland wana tabia ya kuvutiwa na vitega uchumi vya muda mfupi vyenye kiwango kidogo cha hasara; hata hivyo, mradi huu utawatia moyo wa kuzingatia uwekezaji wa muda mrefu ambao unaweza kuwa na manufaa ya kifedha kwa mwekezaji binafsi na jamii.

Pamoja na kusaidia kupunguza kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira katika Somaliland, kutoa vinywaji kwa soko la ndani kutasaidia pia maduka ya rejareja na vya hisani kupata faida kubwa sana, alisema Abdirahman Adam Aar, mhadhiri wa uchumi katika Taasisi ya Watumishi wa Umma.

Aar aliiambia Sabahi kwamba kiwanda hicho kipya kitawasaidia wafanyabiashara kukata gharama ya kuingiza vinywaji kutoka nje. “Watapungukiwa na mzigo wa gharama walizokuwa wakizipata kuingiza vinywaji kutoka Yemen na kuhatarisha meli zenye mizigo yao kuingia mikononi mwa maharamia au kuzama ikiwa na bidhaa zao,” alisema.

Abshir Ahmed Mohamoud, mwenye duka mjini Hargeisa aliiambia Sabahi kwamba ananunua kreti moja yenye chupa 24 za Soda kwa dola 6.40, ambapo alikuwa akitumia dola 11.50 kwa kuingiza kreti moja ya vinywaji kutoka nje. Licha ya kuwa chupa zinazozalishwa ndani ni ndogo, zikiwa na mililita 300 kulinganisha na mililita 500 zinazozalishwa nje, Mohamoud alisema wauzaji wanaonekana kuridhika na bidhaa hiyo.

Kiwanda kipya kitasaidia pia kuongeza mapato mapya kwa serikali. Aar anasema serikali itaweza kutoza kodi kwa bidhaa zinazozalishwa na watu walioajiriwa na kiwanda hicho.

Kuhamasisha uwekezaji Somaliland

Ahmed alisema serikali inapanga kuwaunga mkono wawekezaji wa nje wenye hamu ya kuanzisha viwanda vipya na sekta za uzalishaji.

Alisema serikali iliondoa kodi kwa vifaa na malighafi nyingine zilizoingiza na SBI pamoja na kodi nyengine za bidhaa zinazozalishwa hadi kiwanda kifikie kiwango chake kamili cha uzalishaji.

“Kuanzia sasa, tuko tayari kuendelea na sera ile ile inayohusiana na utozaji kodi wa kuingiza malighafi ambazo ni muhimu kwa uzalishaji wa kiwanda kama ilivyoelezwa kwenye sera ya uwekezaji ya Somaliland. Pia tunaahidi kuondoa kodi katika mauzo ya bidhaa zinazozalishwa na kiwanda kwa miaka mitatu ya mwanzo hadi kifikie uzalishaji kamili na pia kupunguza kodi za bidhaa kwa asilimia 50 kwa miaka miwili inayofuatia,” alisema.

Rais Silanyo alisema utawala wake utafanya kazi na wawekezaji kuendelea kukuza viwanda na kuusaidia uchumi. “Kama serikali, tuko tayari kwa lolote ambalo litahamasisha viwanda kama hiki vitakavyowanufaisha watu wetu kwa kuunda nafasi za kazi,” alisema.

Unaonaje kuhusu makala hii? (Jumla ya Kura 17)

Dislike_icon(3)

(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji

Maoni ya msomaji

  • Yusur
    June 5, 2012 @ 02:30:46AM

    Kusema kweli nimefurahi sana kuona makampuni haya mapya ya Somaliland yanayotengeneza bidhaa na kuwafanya watu wetu waamini kuwa wanaweza kujitengenezea bidhaa zao wenyewe na pia kupata unafuu wa kutosubiri bidhaa za kuagizwa ambazo ziko katika hatari ya kutekwa na maharamia. Mungu ni mzuri. Mwenyezi Mungu yafanye mambo yawe mazuri zaidi kwa ajili yetu.

  • Osman
    June 2, 2012 @ 04:17:14PM

    Haya ni maendeleo mazuri, kwa vile nadhani itatoa nafasi mpya za kazi Somalia yote. Ningependa kuipongeza kampuni ya Coca Cola na mbia wake SBI.

Habari Mpya kabisa

Katika Mwangaza

Jisajili

Kura

Je, unadhania kupigwa marufuku kwa hotuba ya chuki na Tanzania kutakomesha mashambulizi dhidi ya makanisa na misikiti?

Angalia matokeo

Nyenzo