Somaliland yafanya upigaji kura wa mazeozi kupima mchakato wa uchaguzi

Na Barkhad Dahir, Hargeisa

Mei 25, 2012

  • 1 Maoni
  • Chapisha
  • Panga upya Punguza Ongeza

Uchaguzi wa mazoezi uliofanyika mjini Hargeisa wiki iliyopita ulikuwa na mafanikio na umedhihirisha mapungufu muhimu ambayo lazima yashughulikiwe kabla ya raia hawajaelekea kwenye uchaguzi rasmi baadaye mwaka huu, maafisa wameiambia Sabahi.

Uchaguzi huo wa mazoezi ulifanyika tarehe 16 Mei katika makao makuu ya Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kujaribu utaratibu mpya wa uchaguzi, ambao kwa mara ya kwanza utamtaka raia kumpigia kura mtu binafsi na sio chama cha siasa kilicho kwenye orodha, maafisa wa NEC waliiambia Sabahi.

Uchaguzi huo ulifanywa kwa ushirikiano na taasisi ya Interpeace, inayojishughulisha na ujenzi wa amani na yenye makao yake makuu nchini Uswisi.

200 ya wanaume, wanawake, wazee na vijana wenye historia mbalimbali za kielimu walishiriki kwenye zoezi hilo. Washiriki hao walichaguliwa na makundi ya asasi za kiraia kwa ajili ya kuwakilisha uwakilishi mpana, alisema msemaji wa NEC, Mohamed Ahmed Hirsi Gelleh.

Kila mshiriki alipewa dola 10 za Kimarekani na usafiri wa bure kuelekea kituo cha kupiga kura, mpiga kura Muse Yusuf mwenye umri wa miaka 22 aliiambia Sabahi.

Matokeo ya uchaguzi huo wa mazoezi yalionesha kuwa kunahitajika elimu zaidi kwa wapiga kura, kuongezwa kwa wafanyakazi wa tume ya uchaguzi kwenye vituo vya kura na kuongezwa kwa muda wa kupiga kura, ili kujitayarisha kwa uchaguzi ujao wa mabaraza, meneja wa elimu wa NEC, Abdi Osman Haji Abdi, aliiambia Sabahi.

Abdi alisema zoezi hilo limesaidia kujua namna ya kujipanga kwa mfumo mpya wa uchaguzi. “Tulichokikusanya kutoka uchaguzi huu wa mazeozi kitatupa nafasi ya kufanya uchaguzi mzuri [hapo baadaye],” alisema.

Baadhi ya mabadiliko katika upigaji kura yatajumuisha namna ambavyo wagombea watakavyoorodheshwa kwenye karatasi ya kura. Ili kuweza kuchukua idadi kubwa ya wagombea, kila mgombea atakuwa na nambari maalum ambayo itawekwa mahala palipokuwa na nembo ya chama, alisema Gelleh.

“Tungelikuwa tunatumia nembo ya chama cha kila mgombea, basi karatasi ya kura ingelikuwa refu sana [na watu] wasingeliweza kupiga kura [kwa namna hiyo],” alisema Gelleh. “Tulihofia kwamba mabadiliko haya yangeliweza kuwachanganya wapiga kura wasiojua kusoma; tulifanya uchaguzi huu wa mazoezi ili kutathmini inachukuwa muda gani kwa mtu kama huyo kumpigia kura kwa usahihi mgombea anayemtaka.”

Maafisa wa NEC walikuwapo kuhakikisha ikiwa washiriki walijaza karatasi za kura kwa usahihi kulingana na dhamira zao za kupiga kura, alisema afisa wa kituo cha kupiga kura wa NEC, Rabi Sharif.

Abdi aliiambia Sabahi kuwa zoezi hilo limeisaidia NEC kufahamu kiasi gani cha wakati kihitajika ili kupiga kura kwa uhakika, idadi ya watu wanaoweza kupiga kura kwenye kituo kimoja kwa siku ya uchaguzi na idadi ya vituo vya uchaguzi na wafanyakazi inayohitajika.

“Unapokuwa unajitayarisha kwa kazi ngumu na huna uzoefu, njia pekee ya kuifahamu kazi hiyo ni kuijaribu. Kwa hivyo, uchaguzi huu wa mazoezi ulikuwa ni muhimu kwetu kuutayarisha,” alisema.

Siku ya Jumamatu, maafisa wa NEC na wawakilishi wa jumuiya ya Interpeace waliwasili mjini Addis Ababa kuwasilisha kwa wafadhili wa kimataifa yale waliyoyagundua kutokana na uchaguzi huo wa mazoezi na kuchangiana nao makisio yao ya gharama za uchaguzi halisi, alisema Abdi.

Bado tarehe ya uchaguzi haijawekwa, lakini Gelleh alisema kwamba NEC itaweza kutoa tangazo wiki chache zijazo. Tume hiyo inatarajia kuwa uchaguzi utafanyika kabla ya mwisho wa mwaka huu, alisema.

Vyama tisa vya siasa vinatarajiwa kushiriki uchaguzi ujao, vikiwemo vyama vipya vilivyofuzu kupata usajili: Umadda, Wadani, Nasiye, Haqsoor, Rays, na Dalsan. Uchaguzi utafanyika katia wilaya 23 na utakuwa uchaguzi wa tano wa kidemokrasia katika Somaliland tangu mwaka 2002.

Unaonaje kuhusu makala hii? (Jumla ya Kura 12)

Dislike_icon(3)

(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji

Maoni ya msomaji

  • Asha Yusuf
    May 29, 2012 @ 11:11:11AM

    Hili ni zoezi zuri na NEC ilituonesha kuwa wanataka kufanya uchaguzi sahihi wakati wa uchaguzi ujao katika Somaliland. Kwa hivyo tunaweza kusema juhudi za NEC ni nzuri sana. Pia ni nzuri kwa wapiga kura wa Somaliland katika suala la mfumo wao wa kupigia kura.

Habari Mpya kabisa

Katika Mwangaza

Jisajili

Kura

Je, serikali za majimbo ya shirikisho ziundwe vipi nchini Somalia kufuatia utata wa Jubbaland?

Angalia matokeo