Somaliland yaweka mashine za kusafishia damu kwenye figo katika hospitali zake

Na Barkhad Dahir, Hargeisa

Mei 10, 2012

  • 3 Maoni
  • Chapisha
  • Panga upya Punguza Ongeza

Mashine mbili za kusafisha damu kwenye figo zimewekwa huko Somaliland ili kutibu wagonjwa wa figo ambao huko nyuma iliwabidi wakatibiwe nchi za nje.

  • Mgonjwa akipata matibabu ya usafishaji wa damu kwa mashine ya figo katika Hospitali Kuu ya Hargeisa, ambayo ndio pekee nchini Somalia inayotoa tiba hiyo. [Na Barkhad Dahir/Sabahi]

    Mgonjwa akipata matibabu ya usafishaji wa damu kwa mashine ya figo katika Hospitali Kuu ya Hargeisa, ambayo ndio pekee nchini Somalia inayotoa tiba hiyo. [Na Barkhad Dahir/Sabahi]

Mashine hizo mbili zilitolewa kwa Somaliland na Chama cha Hilali Nyekundu cha Jumuiya ya Falme za Kiarabu mwaka 2009, lakini zilikuwa hazijaanza kufanyakazi mpaka hivi sasa.

“Zilikuwa hazijafungwa [kwa sababu], tulikuwa hatuna mtu yeyote [mwenye utaalamu] wa kuzifunga na kutoa mafunzo,” Waziri wa Afya wa Somaliland Dk. Hussein Muhumed Mohamed aliiambia Sabahi.

Alisema wizara iliajiri mafundi wawili na madaktari kutoka India ili kuzifunga na kuziendesha, ikiwa ni sehemu ya misheni ya serikali kupandisha hadhi huduma za afya nchini.

“Kuna mahitaji makubwa Somaliland kwa sababu wagonjwa wengi wenye matatizo ya shinikizo la damu, ugonjwa wa kisukari na uvimbe katika figo wanakuwa na matatizo ya mafigo yao kutofanyakazi vyema, kwa hivyo kuhitaji usafishwaji damu," alisema. “Mashine hizi hazitawarejeshea wagonjwa mafigo yao, lakini zinaweza kutumika kuwatibu kwa sasa.”

Mohamed alisema kwa sasa hakuna mashine nyingi nchini kuweza kutibu idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji usafishaji wa damu. Ili kusaidia kukidhi mahitaji, alisema, mashine za usafishaji damu ambazo mwanzo zilipelekwa Bur’o zitarejeshwa katika Hospitali Kuu ya Hargeisa. Alisema pia serikali inatarajia kupokea mashine nyingine tatu zilizokwisha tumika kutoka serikali ya Uingereza hivi karibuni.

Waziri alisema kuwa serikali inafanyakazi kuhakikisha huduma za afya zinapatikana zaidi. “Tunajaribu tunavyoweza kufanya huduma za afya zipatikane kwa raia wote wenye kipato cha chini na wanaokabiliwa na matatizo ya kupata huduma za afya huko Addis Ababa,” Mohamed alisema.

Dk. Ahmed Weli Dahir, mkuu wa kitengo cha usafishaji damu kwenye figo katika Hospitali Kuu ya Hargeisa, aliiambia Sabahi kuwa wagonjwa kutoka Somaliland walikuwa wanafuata huduma za tiba sehemu kama vile Addis Ababa, Dubai, Malaysia, Djibouti na Nairobi. “Wagonjwa hawa walikuwa wanakabiliwa na gharama za usafiri na matibabu hadi kufikia kiasi cha dola za Kimarekani 5,000,” alisema.

Dahir ni mmoja wa madaktari 30 wa Somalia walioletwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji ili kutoa huduma za afya huko Somaliland.

Dahir alisema kuwa mashine hizo zinafanyakazi kwa siku tatu kwa wiki na zitakuwa zinafanya usafishaji damu kwa wagonjwa sita. “Kila mgonjwa wa figo anayehitaji kufanyiwa usafishaji damu atahitajika kufanyiwa matibabu mara mbili kwa wiki,” alisema, na kuongeza kuwa kila mgonjwa hulipa dola 70 kila anapokwenda hospitali.

Dahir anawapatia mafunzo wataalamu 12 wa nchini humo katika teknolojia ili waweze kushughulikia matibabu hayo badala ya madaktari wageni. Alisema kuwa kwa sasa wako katika mwezi wa pili katika mafunzo ya miezi mitatu.

Ingawaje wagonjwa wengi wa figo wanaweza kufaidika na huduma za usafishaji damu ya figo, bado wanaweza kuziona ada hizo kuwa ni ghali sana.

Laila Jama ni mama wa watoto wanane ambaye mume wake ana matatizo ya shinikizo la damu na alikuwa mgonjwa wa mwanzo kupata huduma za usafishaji damu katika figo mwezi uliopita. Alisema madaktari walimshauri kumpeleka mume wake kwenye matibabu hayo mara mbili kwa wiki kwa muda wa mwaka mmoja.

Lakini Laila, anayeuza mirungi huko Hargeisa, aliiambia Sabahi kuwa hawezi kuzimudu ada za matibabu hayo. “Siwezi kumudu kulipa dola 70 kila mara ninapompeleka mume wangu hospitali kwa usafishwaji damu, kutokana na kipato changu kidogo,” alisema.

Waziri wa afya alisema jumuiya ya wafanyabiashara wangesaidia juhudi za serikali ili kufanya matibabu muhimu yapatikane na yawe na ufanisi kwa kutoa fedha ili kuendesha na kuzihudumia mashine.

“Hatuwezi kuwaambia wale wasioweza kulipa ada za usafishwaji damu wa figo ikiwa hawawezi kulipa,” Mohamed alisema. “Ni jukumu letu kuwapatia huduma za afya. Lazima tutafute msaada kutoka kwa wafanyabiashara ili kutoa misaada kwa hospitali na kutusaida kuuendesha mradi huu.”

Unaonaje kuhusu makala hii? (Jumla ya Kura 12)

Dislike_icon(1)

(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji

Maoni ya msomaji

  • noura
    January 13, 2013 @ 12:56:17PM

    Ninafuraha sana kuona kitu kama hiki nchini mwangu. Ninawaunga mkono mkono watu wangu kwa mafanikio. Hongera sana.

  • Hussein Yusuf
    May 21, 2012 @ 11:59:57AM

    Natarajia kuwa huduma hii itakidhi mahitaji yaliyopo. Ninaamini kuwa huduma hii itawasaidia Wasomali kutoitafuta mahali pengine. Ninawatakia nafuu ya haraka kwa wagonjwa wote.

  • Amina
    May 15, 2012 @ 12:23:09PM

    Nahisi hii ndio huduma nzuri kabisa kutolewa karibuni. Ningependa kuipongeza wizara ya afya ya Somaliland kwa kuanzisha huduma za afya za hali ya juu kama hizi. Ninaiomba wizara kuwatumikia wananchi bila ya kuchoka.

Habari Mpya kabisa

Katika Mwangaza

Jisajili

Kura

Je, unadhania kupigwa marufuku kwa hotuba ya chuki na Tanzania kutakomesha mashambulizi dhidi ya makanisa na misikiti?

Angalia matokeo