Barua ya Bin Laden yafichua uhusiano wa kulazimishwa baina ya al-Qaeda na al-Shabaab

Na Mahmoud Mohamed, Mogadishu

Mei 07, 2012

  • 16 Maoni
  • Chapisha
  • Panga upya Punguza Ongeza

Nyaraka zilizogunduliwa kufuatia kifo cha Osama bin Laden katika maficho yake huko Pakistani zinaonesha uhusiano wa kulazimishwa baina ya al-Qaeda na al-Shabaab.

  • Mpiganaji wa al-Shabaab akiwa amebeba silaha zake wakati wa mazoezi ya kijeshi. Viongozi wa al-Shabaab waliwafanya wapiganaji wao waamini kuwa wameungana rasmi na al-Qaeda, hata hivyo, Osama bin Laden alipinga dhidi ya kushirikiana nao hadharani. [Na Abdurashid Abdulle/AFP]

    Mpiganaji wa al-Shabaab akiwa amebeba silaha zake wakati wa mazoezi ya kijeshi. Viongozi wa al-Shabaab waliwafanya wapiganaji wao waamini kuwa wameungana rasmi na al-Qaeda, hata hivyo, Osama bin Laden alipinga dhidi ya kushirikiana nao hadharani. [Na Abdurashid Abdulle/AFP]

Katika barua ya tarehe 7 mwezi wa Agosti 2010, kiongozi huyo wa zamani wa al-Qaeda alimvunja moyo kiongozi wa al-Shabaab Mukhtar Abu al-Zubayr, anayejulikana pia kwa jina la Ahmed Godane, kwa kutangaza hadharani Jamhuri ya Kiislamu ya Somalia. Bin Laden alimshauri al-Zubayr kuufanya ushirikiano na al-Qaeda kuwa wa siri, na kuutaja uhusiano baina ya makundi mawili hayo kuwa “muungano wa kidugu wa Kiislamu.”

“Ikiwa suala hili litatangazwa na kuwekwa wazi, maadui wenu wataongeza shinikizo na kujiimarisha dhidi yenu; haya ndiyo yaliyotokea kwa ndugu zetu wa Iraki na Algeria,“ bin Laden aliandika.

Bin Laden pia alisema uhusiano wa wazi na al-Qaeda ungewavunja moyo wafanyakazi wa Kiarabu katika kuwasaidia Wasomali na kungetia doa uhusiano baina ya wanamgambo na watu wa Somalia.

Ahmed Sheikh Hussein, mchambuzi wa kisiasa juu ya makundi ya Waislamu wenye itikadi kali nchini Somalia, alisema barua inaonesha mgawanyiko baina ya makundi mawili.

“Nyaraka hizi zinajenga taswira kuwa bin Laden hakuwa anapendezwa na al-Shabaab na pia inaonesha kuwepo kwa ushirikiano wa kulazimishwa baina ya al-Shabaab na al-Qaeda wakati wa bin Laden kuhusiana na al-Shabaab kujiunga na al-Qaeda,” alisema.

Hussein alisema bin Laden alikuwa ana shauku juu ya al-Shabaab, hata kama kikundi hicho kiliapa uaminifu kwake mwaka 2009. “Hii inaweza kuwa kwa sababu ya imani yake kuwa utendaji wa al-Shabaab ulikuwa unafanya makosa na kwamba ulikuwa unashadidia sana juu ya kulazimisha Sharia, bila ya kutaja kuongezeka kwa migawanyiko ya ndani miongoni mwa viongozi wake,” aliiambia Sabahi.

Vyombo vya habari nchini wakati huo uligusia kuwa al-Shabaab walikuwa ukingoni mwa kutangaza Jamhuri ya Kiislamu nchini Somalia, licha ya mwongozo wa bin Laden. “Mwezi Disemba 2010, al-Shabaab ulikuwa karibu na kubadilisha jina kuiita 'Jamhuri ya Kiisalamu ya Somalia' baada ya mkutano wa siri miongoni mwa viongozi wa kikundi katika mji wa Somalia wa Merca katika kujadiliana juu ya hatima ya al-Shabaab,” Hussein alisema.

Alisema kuwa makundi mawili hayo yalikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara kupitia wanachama wa al-Shabaab waliokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na uongozi wa juu wa al-Qaeda au kupitia kwa wajumbe wa al-Qaeda waliokuweko Somalia.

“Licha ya kuwepo mvutano baina ya pande mbili hizi, al-Shabaab walipokea ushauri na mafunzo kutoka kwa wanachama wa al-Qaeda na kujaribu kujihisi kama ni washirika wa al-Qaida badala ya kuwa tawi kuu la shirika lao,” Hussein alisema.

Viongozi wa al-Shabaab waliwaficha wapiganaji wao juu kukataliwa kwao

Viongozi wa al-Shabaab walimshawishi bin Laden kubadili uamuzi wake na kuwaficha wapiganaji wao, alisema Abdirahman Abdullahi, mtafiti wa masuala ya al-Shabaab katika Kituo cha Huduma za Vyombo vya Habari Somalia.

“Ingawaje viongozi wa al-Shabaab – au angalau baadhi yao – walijua juu ya msimamo wa bin Laden, wakati ilipokuja kukataliwa kwa kuyafanya mahusiano hayo hadharani…waliwafanya wapiganaji wao wahisi kuwa uhusiano na al-Qaeda ulikuwa mzuri na kwamba wao walikuwa sehemu ya al-Qaeda katika Pembe ya Afrika,” Abdullahi aliiambia Sabahi. “Walifanya hivi ili kuendeleza mori miongoni mwa wapiganaji waliokuwa wanamchukulia bin Laden kuwa ni kiongozi wa kiimani na wa kuigwa katika masuala yanayohusiana na jihadi.”

“Kwa sababu hii, viongozi wa al-Shabaab walisisitiza kuwa kiongozi wao mkuu alikuwa bin Laden na waliweza kutoa hotuba na rekodi zenye jina, ‘Tunasikiliza wito wako, Osama’, ‘Tuko kwa kukuhudumia, Osama’, ‘Sisi ni wafuasi wako katika Pembe ya Afrika’, na mambo kama hayo,” alisema.

Kukataa kwa bin Laden kulizusha mgawanyiko

Kukataa kwa bin Laden kulisababisha ufa miongoni mwa viongozi wa al-Shabaab, mchambuzi wa kisiasa na profesa wa chuo kikuu Mohammed Ahned aliiambia Sabahi.

“Inaonesha kuwa kukataa kwa bin Laden ombi la al-Shabaab kujiunga na al-Qaeda kulisababisha hasira miongoni mwa [baadhi ya] viongozi wa kikundi,” Ahmed alisema. “Walilichukulia hili kama kwamba kiongozi wa al-Qaeda hakuwa na shauku ya kukubali uanachama wa al-Shabaab, kwa hivyo kuona ni bure kwao kuimarisha itikadi za al-Qaida.”

“Kwa sababu hii, viongozi wa al-Shabaab wakagawanyika katika kambi mbili: moja ile iliyokuwa na msimamo mkali na kutaka kuungana na al-Qaeda kama njia ambayo ilimfaa kiongozi wake, na ya pili ilikataa kujishughulisha na al-Qaeda ikiwa kiongozi wake alikataa kuungana rasmi baina ya pande mbili hizo,” alisema.

Ahmaed alisema mgawanyiko wa ndani uliendelea mpaka pale bin Laden alipouliwa, ndipo kulipowapo fursa ya al-Shabaab kujiunga na al-Qaeda, kwa sababu kiongozi mpya wa al-Qaeda, Ayman al-Zawahir, hakufuata tena njia aliyokuwa anayofuata mtangulizi wake juu ya washirika wa al-Qaeda.

Barua inayoaminiwa kuandikwa na al-Zawahiri mwezi Desemba 2010 na kutolea pamoja na barua kutoka kwa bin Laden, ilimtaka bin Laden kufikiria upya msimamo wake kuhusu kuwaunganisha al-Shabaab kwa sababu “hakuna haja ya kuwakatalia”.

Al-Zawahiri alitangaza rasmi muungano wa al-Shabaab na al-Qaeda mwezi Februari 2012. Muungano huo unaaminiwa umeleta mgawanyiko zaidi baina ya viongozi wa al-Shabaab, ikiwa ni pamoja na uasi wa wazi na kupoteza kuungwa mkono na umma kufuatia operesheni zao za kuwalenga raia.

Barua ya Bin Laden itawachanganya wanamgambo wa al-Shabaab

Kutolewa kwa barua ya Bin Laden kutawachanganya zaidi viongozi wa ngazi za chini na wanamgambo wa al-Shabaab, alisema Ahmed.

“Kwa upnde mmoja, wanamgambo watashangaa kwa nini uongozi wao wa juu ulilazimisha mnasaba wao na bin Laden, wakati yeye mwenyewe hakuwa akipendelea wazo la makundi hayo kujiunga pamoja rasmi,” alisema. “Kwa upande mwengine, uongozi wa juu wa al-Shabaab watawageukia wapiganaji wao kwa kuwaambia kuwa nyaraka hizi ni za uongo na ni sehemu ya propaganda za maadui wa mujahidina hao kama njia ya kuoandikiza mgongano baina yao.”

“Licha ya mahusiano baina ya makundi haya mawili, al-Shabaab imekuwa sehemu rasmi ya al-Qaeda,” alisema. “Kuiweka al-Shabaab chini ya mwamvuli wa al-Qaeda kunaweza kuwa jaribio la kupandisha mori ya wapiganaji wake, kwa sababu hatua hii ilikuja wakati ambapo al-Shabaab ilikuwa inashuhudia kushindwa na kurudishwa nyuma vibaya yakiwa matokeo ya kampeni ya pamoja ya nchi za Pembe ya Afrika dhidi ya kundi hilo."

Unaonaje kuhusu makala hii? (Jumla ya Kura 49)

Dislike_icon(13)

(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji

Maoni ya msomaji

  • abdiqadir isgow
    July 17, 2012 @ 08:18:05AM

    Tumeona kwamba al-Qaeda inawalenga wananchi wasio na hatia katika nchi za Mashariki ya Kati. Watu wengi wanajiuliza kwa nini kikundi hiki kiliacha kupigana na serikali yenye silaha na kuwaelekea raia. Tendo lao linaweza kuwa limechangiwa na vitu vingi ambavyo inawezekana vimetokea baada ya kifo cha bin Laden. Kikundi kimepoteza njia zake kuu za kupatia fedha na sasa kinawalenga raia ambao wana uwezo ili kudai pesa za kuwakomboa. Kikundi kinazidi kuchanganyikiwa kwa sababu hawana pesa na pahali pekee wanakoweza kuzipata ni kuwateka raia matajiri. Aina nyingine ya watu ambao al-Qaeda inawalenga ni maafisa wa usalama wa vyeo vya juu. Si lazima hawa wawe lengo lao, wanakodiwa na baadhi ya maofisa matajiri ambao hawataki kuwepo kwa mazungumzo ya amani. Kwa ufupi ni kuwa kikundi kimegeuka kuwa cha askari wa kukodiwa na wezi maarufu wanaofanyakazi kwa mahitaji yao ya kichoyo na raia ndio upande unaoumia.

  • yaser hussein mazi
    July 12, 2012 @ 04:55:11AM

    Kama kilivyo kikundi chochote cha kigaidi, kila unapomuua kiongozi kutoka kikundi chochote, kikundi kinakuwa kinapoteza udhibiti na kuanza kuvunjika. Huu ndio uliokuwa mpango wa Wamarekani, kwa vile walijua kuwa mara tu unapomuua mwamba wa al-Qaeda, kwa hivyo itakuwa rahisi kwa kikundi kudondoka chini. Sababu nyingine kwa nini mauaji ya kiongozi kulileta mwanga kidogo kuelekea kuifikisha Al-Shabaab mwisho wake kwa sababu, al-Qaida walikuwa wanapokea amri moja kwa moja kutoka kwake. Hii ilimaanisha kuwa kama bin Laden angekuwa bado anaishi, angeweza kuendelea kuongoza na kuonesha wapi rahisi pa kupiga bomu.

  • snichchisky
    July 3, 2012 @ 09:49:40AM

    Al-Shabaab wangeacha kupigana kwa sababu serikali ya Kenya imewakamata. Tayari wamechelewa sana kwa wao kupigana. Kadiri askari wanavyokuwa wengi, ni bora.

  • John
    July 2, 2012 @ 09:41:29AM

    Maoni niliyosoma kuhusiana na watu wa Somalia na al-Shabaab napata picha ya hali mbili zisizo za kweli. Kwanza, mimi ni Mkenya, na kwa kiasi cha muongo uliopita, nimeishi pamoja na watu wa Somalia kwa amani, kwa njia ya upendo. Ni watu wastaarabu, wanaopenda amani na wanatetea maisha ya kibinadamu kama mtu yeyote ulimwenguni kote. Dini [ya Kiislamu] inatetea mila hizi vile vile. Al-Shabaab ni kikundi cha wahalifu tu wanaojificha nyuma ya mafundisho ya udanganyifu na kuyatetea kama kwamba ni mafundisho ya kweli ya Kiislamu, jambo ambalo sio kweli. Hakuna dini ambayo inafundisha kuepuka na hata kuharibu maisha ya binadamu wengine hata wakati mtu anamwabudu Mungu wetu, aliyetupa maisha. Al-Shabaab, hamtashinda. Acheni vitendo vyenu vya kinyama au Mwenyezi Mungu atawasimamisheni.

  • ALLAH IS ONE AND MOHAMED IS MESSENGER OF ALLAH
    June 19, 2012 @ 07:11:35PM

    SI WATU WOTE WASOMALIA NI MAGAIDI........

  • Mikhail
    June 18, 2012 @ 09:18:39AM

    Osama bin Laden alikuwa mtu wa mbinu kwa kiasi fulani, kwa sababu idadi kubwa ya vikundi na wapiganaji, na kwa hivyo kuacha alama nyingi nyuma yao. Nisingependa kujihusisha na masuala ya kidini, hata hivyo, neno JIHADI katika maana ya Kiislamu linatumika vilivyo. Uislamu ni dini ya amani na Mwenyezi Mungu si ndugu yako aliye dhaifu au jamaa yako unayetaka kumsaidia. Uislamu hauvumilii vurugu za aina yoyote, achilia mbali kupoteza maisha ya wasiokuwa na hatia. Vikundi vyote hivi ni vigenge vilivyoundwa na kujificha nyuma ya dini na ujinga wa wafuasi wao. Ni kazi ya wachache ambao kwa maoni yangu wana siasa kali na wanatumia fursa ya machafuko katika mataifa ya Kiislamu. IKIWA UISLAMU kweli ni dini ya AMANI, kwa hivyo kusiwepo na vurugu na vifo visivyo vya lazima. Yanayojiita mataifa ya Kiislamu lazima yawe mfano wa amani, kama mataifa yanayopenda amani chini ya misingi ya Uislamu na nguzo zake. AMANI IWE JUU YENU.

  • Newton
    June 18, 2012 @ 02:48:30AM

    Ninakubaliana sana na Bishar Hajji kuhusu maoni ya Cathereen juu ya jamii ya Somalia. Haina mantiki kufikiria kuwa katika enzi hii binadamu mwenzako anaiita jamii nzima kuwa ni ya kijinga na ya kishenzi. Angehisi vipi ikiwa kosa la mtu mmoja au kikundi fulani, litachukuliwa kama kosa la jamii yote. Hapo ndio tunaweza kuiita jamii kuwa ni ya wajinga, magengi na wasiotakiwa. Kuwa ndugu wa kuwatetea ndugu zako. Tuwe na hadhari juu ya kile tunachosema.

  • kepher ondere
    June 17, 2012 @ 01:53:02PM

    Wasomali wapigane kwa ajili ya taifa lao na kuungana na ulimwengu wote ili kuboresha maisha yao wenyewe. Wakati umekwisha kwa vikundi vyenye itikadi kali na kwenda mstari wa mbele wa kuboresha uchumi wao na wasifuate mwenendo wa kukosekana kwa amani katika kanda hii.

  • Jonas
    May 24, 2012 @ 03:15:17AM

    Mimi ni Mtanzania. Nimeishi miaka yangu mingi bila kuoa damu ya mwaadamu ikimwagwa na mwanadamu mmwenzake kwa kupenda tu. Ila damu zinazoendelea kumwagika ni kwa njia ya ajali za vifaa vya moto kama magari,pikipiki na treni. Kweli ndugu zangu wa somalia mnaimwaga damu ya Baba Yenu, Kisha ya Mama Yenu, Kisha Ya Wadogo zenu, Tena haitoshi mnasababisha na damu ya wanawenu kumwagika. Siamini kuwa dini ya waislamu inaruhusu matendo hayo.La! Hashaa! Ninawaomba wananchi mliopo somalia mpambane bega kwa bega na serikali yenu kuwakabili hao wanaojiita al-Shabaab msiwaogope ni watu kama nyinyi. Njia za kupambana na hao ni ndogo sana wala hazihitaji siraha za moto kupambana nao; SISI HUKU TANZANIA TUNA SIRAHA 1 YA KUPAMBAMBANA NA MAADUI KAMA HAO, Siraha hiyo ni "Kila mmoja awe polisi wa mwenzake". hii ina maana gani? Jirani yako unajua kuwa ni mwanakikundi cha al-Shabaab basi jikongoje/nenda kimya kimya kwenye chombo cha sheria/dola (Polisi) na umtaje huyo mtu kwa jina, matendo na tabia zake uwape polisi adresi yake namba ya simu ukiweza wape barua pepe yake na taarifa zozote za kiusalama. Sio lazima uwe na uhakika nae kuwa ni al-Shabaab la! ila tu ukiona anamuonekano usioeleweka kama vile yeye huwa anafanya shughuli zake kwa maficho, ana pesa zisizoeleweka zina toka wapi, hana kazi inayoeleweka na kutambulika. Ewe Baba,Mama,Kaka,Dada wasomali tumieni hii njia kuwateketeza sio tu al-Shabaab bali hata makundi na watu wa namna hiyo. KUWA POLISI WA MW

  • Bishar haaji
    May 15, 2012 @ 09:53:06PM

    @Cathryn. Ninashangazwa kuwa maoni yako yanachapishwa licha ya maoni yako ya kukera juu ya Wasomali. Sio siri na nisingesita kukuita mjinga na mbaguzi. Kuihukumu Somalia kwa kinachoendelea kwa muda wa miongo miwili iliyopita ni hoja ya uongo, huko nyuma ilikuwepo Somalia nzuri, imara na yenye mafanikio iliyokuwa na uhuru kuliko nchi nyingi za Kiafrika kutoka ANC hadi Angola. Mimi ni Msomali na nimekuwa nikiota Somalia iliyo huru bila ya ugaidi. Ndio, mimi naamini taifa linaloendeshwa bila kufuata dini. Al-Shabaab ni wajinga kama walivyo viongozi wao. Mtu mmoja mwenye busara alisema kipofu hawezi kumuongoza kipofu. Gaidi marehemu Osama alikuwa kipofu, alikuwa na upofu wa uhuru, upofu wa amani, upofu wa haki za binadamu, hivyo hivyo ndivyo walivyo al-Shabaab. Kwa hivyo unachokiona katika makala hii ni mawasiliano baina ya magaidi wawili wasiohuruma na wapenda damu. Na ninashangazwa unashabikia kikundi kimoja cha kigadi kama vile al-Qaeda kwa kutokiunganisha kikundi kingine cha mtandao wa kigaidi, al-Shabaab, kwa sababu unafikiri hawa wa mwisho ni wajinga. Ninakubaliaana nawe kuwa wote ni wajinga na watu wasio na ubinadamu. Lakini kwa kuwachanganya al-Shabaab na Wasomali hakufai kwa sababu vikundi hivi vilituzuwia uhuru wetu, vilituua, na kusababisha kutokuwapo na utulivu kikanda. Kwa hivyo ninakutaka utoe maoni ya kistaarabu na ya kibinadamu na useme nina ndoto ya Somalia iliyo bora zaidi kwa taifa hili la washairi kama linavyojulikana litasimama tena, kutoka wimbo wa taifa ni tunapokuwa wazee ndipo tunapokuwa imara zaidi, watatuita huru kama bendera inayopepea.

  • Mr. ileeye
    May 13, 2012 @ 02:49:58AM

    Tuepuke mauaji ya watu ambao hawana silaha. Tumeonywa na Mungu dhidi ya umwagaji damu ya watu wasio na hatia.

  • Fanah ali
    May 12, 2012 @ 07:06:32AM

    Ningesema kuwa kumekuwepo na mabadiliko kidogo katika mbinu za kikundi cha kigaidi cha al-Qaeda tangu kufariki kwa Osama bin Laden. Kumekuweko na mabadiliko ya kiongozi na mabadiliko ya uongozi lakini kikundi kimegeuka kutoka kile kilivyokuwa kabla. Kimegawika katika vikundi vidogo vidogo vyenye maslahi binafsi na visasi vya kulipiza. Hawapigani vile vita ambavyo mwanzo vilikuwa vita vitakatifu, sasa wamekuwa majambazi wanaotaka kujitajirisha wenyewe. Magaidi wa al-Qaeda sasa wanateka nyara watu matajiri na kutaka wapewe pesa nyingi. Kikundi hiki pia kinafanyakazi ya uaskari wa kukodiwa na wanafanya mauaji kwa ajili ya pesa. Kwa hivyo ningesema kuwa mbinu zimebadilika tangu kifo cha bin Laden lakini kikundi hiki bado ni tishio la kimataifa.

  • Bearth
    May 11, 2012 @ 09:22:38AM

    Wanapigana kwa kujimaliza wenyewe na niw akati tu ndio utakaoamua. Hakuna dini inayoruhusu kumuua binadamu mwenzako. Hawa wanalazimika kuangamia isipokuwa tu kama wataona mwangaza.

  • Jm
    May 9, 2012 @ 10:19:21AM

    Kwa nini wanalibadilisha taifa lote kuwa kama kikundi ovyo ovyo, ambapo taifa lilitarajiwa kupigana na wageni na sio kupigana wenyewe. Je, ni kwa ajili ya pesa? Natumai kuwa sasa Wasomali watajiangalia wenyewe.

  • Mohammed
    May 9, 2012 @ 02:58:35AM

    Al-Shabaab imekufa. KDF na EDF endeleeni kuwaua!!!

  • cathrynnozickbmxs
    May 8, 2012 @ 04:55:23AM

    Waarabu ni watu waliostaarabika (Wastarabu) wakati Wasomali ni watu wenye heshima mbovu, wabaya na kwa kawaida ni jamii ambayo inajiendesha kijingajinga...ni wazi kuwa kiini cha wanajihadi wataepuka kujiunga na watu waliochanganyikiwa kama Wasomali. Hii ni kusema kwamba al-Shabaab si kikundi cha jihadi bali genge lenye kiu ya damu, genge la waathiriwa wa madawa ya kulevya, genge la uhalifu la Kiislamu, linalojihusisha na ubakaji, kutweza watu nguvu na kuwanajisi wanawake wao wenyewe, wavulana na wazee. Jumuiya ya kimataifa lazima iwalazimishe Wasomalia waishi nchini mwao, inabidi warejeshwe, wakataliwe uraia na warejeshwe kwenye nchi yao yenye vumbi na joto ili majambazi hawa wakabane roho wao kwa wao katika vitendo vyao wenyewe vya kihalifu, kwa vile watu wabaya hawa wameamua kufuata itikadi ya kujiamini wenyewe kuwa ni Ufalme wa Somalia...tafadhalini Wasomali...Nendeni mkauimbie upepo!

Habari Mpya kabisa

Katika Mwangaza

Jisajili

Kura

Je, unadhania kupigwa marufuku kwa hotuba ya chuki na Tanzania kutakomesha mashambulizi dhidi ya makanisa na misikiti?

Angalia matokeo