Viongozi wa Dhusamareb waongeza usalama baada ya shambulio la al-Shabaab

Darmaan Farah Adde wa Puntland na Mahmoud Mohamed wa Mogadishu walishiriki katika ripoti hii

Mei 04, 2012

  • + Toa maoni sasa
  • Chapisha
  • Panga upya Punguza Ongeza

Viongozi wa Ahlu Sunna wal Jamaa (ASWJ) wameongeza hatua za usalama huko Dhusamareb kufuatia shambulio la kujitoa muhanga katika mgahawa ambalo liliua watu sita na kuwajeruhi vibaya sana watu wengine zaidi ya kumi hapo Jumanne (tarehe 1 Mei).

Hatua hizo za usalama zilizoimarishwa ni pamoja na amri ya kutotoka isiyo na kikomo kutoka magharibi hadi alfajiri pamoja na kuongeza idadi ya vituo vya ukaguzi barabarani maeneo ya mjini, makamu kiongozi wa ASWJ Sheikh Ahmed Abdullahi Ilkaase aliiambia Sabahi. Wanamgambo hao wanaoiunga mkono serikali wanaongoza baadhi ya sehemu za jimbo la Galguduud.

Wabunge walikutana na raia katika mgahawa ili kuzungumza uanzishaji wa utawala wa mkoa, wakati kijana wa kiume alipoingia na kujilipua, kwa mujibu wa maafisa na mashuhuda. Raia wanne na wabunge wawili waliuawa, na wabunge wengine wawili walikuwa kati ya majeruhi.

“Mtu aliyejilipua mwenyewe alikwenda karibu na eneo ambalo maafisa hao walikuwa wamekaa kwenye duka la kahawa na kujilipua wakati alipokamatwa na mmoja wa maafisa wa usalama wa wabunge,” Duraan Ali Jama, mkazi aliyeshuhudia mlipuko aliiambia Sabahi.

Hali ya majonzi ililikumba eneo hilo mara baada ya mlipuko, alisema.

Maafisa wa ASWJ waliiambia Sabahi kuwa walishangazwa sana na shambulio hilo.

“Ni mkakati mpya. Tumekuwa tukipambana na wanachama wa al-Qaeda katika eneo hili tangu zamani… lakini kazi hii ya kuwalenga watoto na maeneo ya umma ni njia mbaya na itapelekea kuvunjika kwao,” Ilkaase alisema.

Al-Shabaab walidai kuhusika na shambulio hilo na kulielezea kuwa ni tendo la kulipiza kisasi kwa kifo cha Adaan Haji Eyrow, afisa mkuu wa kikundi aliyeuliwa huko Dhusamareb mwaka 2008.

“Mtu aliyemuua Adaan haji Eyrow ni mmoja wa watu waliouliwa huko Dhusamareb. Mungu ametuwezesha kuwaua katika njia waliyopanga kumuua Adaan miaka minne iliyopita,” alisema msemaji wa al-Shabaab Sheikh Ali Mohamud Rage, alipokuwa akizungumza na Redio Andalus inayodhibitiwa na al-Shabaab hapo Jumanne jioni.

Wabunge Yusuf Mire Seerar na Abdiweli Mohammed walikuwa miongoni mwa wahanga waliofariki. Siku ya Jumanne, baadhi ya waathirika walionusurika walisafirishwa kwenda Addis Ababa kwa matibabu. Wengine walipangiwa kupatiwa matibabu mjini Nairobi.

Serikali ya Somalia na viongozi wa mkoa wa eneo hilo walilaani shambulio hilo na kuapa kuendelea na juhudi zao za kuwang’oa al-Shabaab kutoka Somalia.

“Al-Shabaab na al-Qaeda wameamua kuua raia wa Somalia na wanazuoni wake, lakini hawataizuia serikali kutokana na juhudi zake za kuwamaliza al-Shabaab,” Waziri wa Habari wa Somalia Abdikadir Hussein Mohammed alisema katika taarifa.

Waziri aliwataka raia kuungana dhidi ya ugaidi wa al-Qaeda.

Sheikh Nur Barud Gurhan, msemaji wa Jumuiya ya Wanazuoni wa Somalia, alilaani shambulio hilo la kujitoa muhanga na kuviita vitendo vya al-Shabaab kuwa “si vya Kiislamu,” uliripoti Mtandao wa Habari wa Shabelle.

Sheikh Mohammad Yusuf Hefow, mkuu wa ASWJ, alituma rambirambi zake kwa familia za wahanga na kusisitiza kuwa ASWJ inaahidi kuhakikisha usalama katika eneo lililo katika udhibiti wake.

“Walichofanya kikundi cha kigaidi cha al-Qaeda ni kitendo cha kikatili,” Hefow alisema, na kuongeza kuwa watachunguza wapi shambulio hilo lilipangwa.

Omar Ali Roble, waziri wa kuwanyang’anya silaha na kuwarejesha wanamgambo katika maisha ya kawaida, aliiambia Sabahi kuwa ujumbe wa serikali unachunguza eneo lililolengwa na shambulio hilo.

Roble, ambaye ni sehemu ya ujumbe huo, alisema wanatembelea maeneo yaliyokombolewa karibuni kutoka kwa al-Shabaab ili kujadiliana na viongozi wa maeneo njia bora za kuunda serikali ya mkoa na kutoa usalama katika maeneo hayo.

“Shambulio hilo lilikusudiwa wajumbe wanaofanya ukaguzi katika eneo,” Roble alisema. Al-Shabaab wamefeli, [shambulio] halikufichua lolote kwani wao waliwatangulia,” alisema.

Unaonaje kuhusu makala hii? (Jumla ya Kura 8)

Dislike_icon(1)

(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji

Habari Mpya kabisa

Katika Mwangaza

Jisajili

Kura

Je, unadhania kupigwa marufuku kwa hotuba ya chuki na Tanzania kutakomesha mashambulizi dhidi ya makanisa na misikiti?

Angalia matokeo