Aprili 25, 2012
Kukiwa na mvua kubwa tayari inanyesha karibu nchini kote, Wakenya waliohama makazi yao wakati wa vurugu za baada ya uchaguzi zaidi ya miaka minne iliyopita, wameonesha wasiwasi wao kuhusu matatizo ya kibinadamu yanayowakabili wakati wakisubiri kupatiwa makazi mapya.
Maafisa wa Kenya wanasema hatua za kufaa zimechukuliwa ili kuhakikisha kuwa watu waliokimbia makazi yao hawateseki wakati wa msimu wa mvua, ambapo wawakilishi wa watu hao waliiambia Sabahi kuwa serikali na wadau wa maendeleo wanapaswa kuchukua hatua haraka ili kuepuka matatizo makubwa ya kibinadamu.
Mkuu wa Mkoa wa Bonde la Ufa Osman Warfa, ambaye anahusika na mpango wa makazi kwa watu waliokimbia makazi yao, aliiambia Sabahi kuwa serikali imechukua hatua zinazofaa ili kuhakikisha watu hao wanapata mahitaji yao ya msingi katika makambi kabla ya kupatiwa makazi mapya sehemu nyingine.
“Mwanzoni, kulikuwa na matukio ya msongamano wa watu na usambazaji maji usiofaa. Kutokuwepo kwa majengo ya kutosha ya usafi katika baadhi ya kambi kuliwafanya watu waliokimbia makazi wawe rahisi kupata magonjwa, lakini matukio kama hayo sasa ni kidogo sana,” Warfa alisema.
Bonde la Ufa ilikuwa mmoja wa mikoa iliyoathiriwa na vurugu za baada ya uchaguzi wa 2007 na inao wengi wa watu waliokimbia makazi yao, kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa mwaka jana na Tume ya haki za Binadamu na Mtandao wa taifa wa watu waliokimbia makazi yao.
Kwa mujibu wa Wizara ya Programu Maalumu, vurugu za baada ya uchaguzi zilipelekea watu 663,921 kukimbia makazi yao. Kati ya hao, watu 350,000 walichagua kukimbilia katika kambi 118, wakati watu 313,921 walichanganya na jamii zao Kenya kote.
Wizara ilisema familia 4,885 bado zahitaji kupatiwa makazi mapya.
Katika wilaya ya Naivasha, karibu kilomita 50 kaskazini magharibi ya Nairobi, kuna kambi kumi za watu waliokimbia makazi yao zinazo toa makazi kwa zaidi ya familia 1,500 kwa jumla. Hata hivyo, ni kambi tano tu ambazo zimetambuliwa na serikali, Mkuu wa Wilaya ya Naivasha Hellen Kiilu aliiambia Sabahi.
Kiilu alisema kambi zilijengwa kwa ajili ya watu waliokimbia makazi yao waliochagua kuishi katika kambi au waliochukuliwa na marafiki au ndugu zao. Badala ya kujiunga na kambi rasmi zilizowekwa. Watu mmoja mmoja baadaye walinunua ardhi kwa pamoja na kuanzisha kambi zao wenyewe kwa msaada wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na watu wema wakati wakisubiri kutafutiwa makazi mapya na serikali, alisema.
Serikali inasema kambi kama hizo zisizo rasmi hazina sifa za kupata msaada wa serikali.
“Tuliweka tarehe ya mwisho ya kuwaandikisha watu wote waliokimbia makazi yao, ambayo ilikuwa tarehe 31 Disemba, 2008 na hizo ndizo takwimu tunazotumia. Mtu yeyote aliyeweka kambi binafsi baada ya tarehe ya mwisho haziwezi kutambuliwa na serikali,” Katibu Mkuu wa Wizara ya Programu Maalumu Andrew Mondoh aliiambia Sabahi.
Wizara ya Programu Maalum inatoa mgao wa chakula kwa watu katika kambi zinazotambuliwa, lakini wengine wanasema hautoshi.
Beatrice Nyokabi, mwakilishi wa kambi ya Ebenezer inayotambuliwa na serikali, anasema familia zilizokimbia makazi yao zimepata usumbufu usiosemekana katika miaka minne iliyopita.
"Kwa sisi, ni usumbufu unaoendelea na tunahofia kuwa tunaweza kusahauliwa wakati siasa na uchaguzi mkuu ujao vimekuwa vitu pekee vinavyozungumzwa kila siku,” aliiambia Sabahi.
Rose Wanjiku, mwakilishi wa kambi ya Jikaze, alisema vijana wengi katika makambi hayo wameacha shule kutokana na hali ya hewa mbaya na kwa kutembea masafa marefu.
“Hatuna mfumo wa kuaminika wa usafiri hapa na shule ya karibu ipo umbali wa kiasi cha kilomita tano, jambo ambalo si rahisi kwa watoto wadogo,” Wanjiku alisema.
Watu waliokimbia makazi yao wenye maradhi makubwa kama vile VVU/UKIMWI, pia wanaishi katika hali mbaya kwa sababu hawapati chakula kizuri cha kuweza kuwasaidia kuhimili madawa makali wanayoyategemea, alisema. “Kwa watu hawa, hata kujipatia mlo mmoja ni tatizo, na matokeo yake ni idadi wao kubwa wameshakufa,” alisema.
Wanjiku alisema vituo vya tiba pia viko mbali kutoka makambini. “Hospitali ya karibu ipo umbali wa kilomita 30, na tumewashuhudia baadhi ya watoto wakifa kwa sababu hatuwezi kuwakimbiza hospitali, hasa wanapougua usiku,” alisema.
Mbunge wa Naivasha John Mututho alisema watu waliokimbia makazi yao wana huduma chache katika jimbo lake. Alisema kiasi cha watu watatu hufa kila mwezi na shule na hospital za karibu zimezidiwa.
"Serikali imetumia fedha nyingi kwa watu hawa, lakini hatuoni mabadiliko yoyote, kwa vile wahanga wanaendelea kuteseka,” Mututho aliiambia Sabahi.
Kamati ya bunge iliyoteuliwa kutathmini hali za programu ya makazi ya watu waliokimbia makazi yao iligundua kuwa Wizara ya Programu Maalumu haikufanya mengi katika kuwapatia makazi mapya watu hao, mwenyekiti wa kamati Ekwe Ethuro aliiambia Sabahi.
Lakini Msaidizi wa Wizara ya Programu Maalumu Mohamed Gabbow aliiambia Sabahi kuwa kazi ya wizara inaendelea vyema. Alisema kuwa mpaka kufikia mwezi wa Disemba 2012, serikali ilikwishatumia shilingi bilioni 10 (sawa na dola za Kimarekani milioni 120) kwa kuwapatia watu watu waliokimbia makazi yao makazi mapya.
Alisema serikali tayari imeshawasaidia baadhi ya watu waliokimbia makazi yao waliorejea katika mashamba yao ili kuanza maisha yao upya.
“Hatua zinazofaa tayari zimewekwa na serikali inafanyakazi na wadau kadhaa wa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kuhakikisha kuwa kambi za watu waliokimbia makazi yao zinafungwa na kila mtu anapatiwa makazi kabla ya uchaguzi kufanyika,” Gabbow alisema.
Tom Ondicho, mhadhiri katika Taasisi ya Masomo ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alisema pamoja ya kuhakikisha huko kwa maafisa, serikali lazima ifanye kazi kwa ufanisi pamoja na wadau wa maendeleo ili kutoa fedha na nguvu-watu ili kupata suluhisho la kudumu la tatizo hili.
"Ingawaje kumekuwepo na hatua kubwa ili kuhakikisha hifadhi na msaada wa watu waliokimbia makazi yao, mchakato umechukua muda mrefu sana, na kwa kuwa nchi inajitayarisha na uchaguzi ujao…kupatiwa kwao makazi mapya kunapaswa kupewe kipaumbele ili kuepuka tatizo jengine, aliiambia Sabahi.
Uchaguzi mkuu ujao wa Kenya umepangwa kufanyika mwezi Machi 2013.
Raisi wa Kenya Uhuru Kenyatta siku ya Alhamisi (tarehe 23 Mei) alitoa majina mawili ya mwisho ya ...
Watu watano waliuawa na wanne kujeruhiwa katika mashambulizi mawili kwenye eneo la kaskazini mash...
Sababu kuu ya vurugu ambazo ziliua zaidi ya watu 150 katika Delta ya Mto Tana mwaka jana ilitokan...
Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa polio katika Pembe ya Afrika siku ya Jumatan...
Majeshi ya serikali ya Somalia yamezifungia kampuni za mawasiliano ya simu na biashara nyingine h...
Serikali ya Somalia itaanza kuunda tawala za kikanda katika maeneo yaliyokombolewa kutoka kwa al-...
Waziri wa Nishati wa Djibouti Ali Yacoub Mohamoud na Balozi wa Japani nchini Djibouti Atsushi Nis...
Ufunguzi wa Mkutano wa Wasambazaji wa mafuta na gesi Tanzania utafanyika huko Dar es Salaam tareh...
Wabunge wameondoa hoja yao inayomtaka Waziri Mkuu Abdi Farah Shirdon na baraza lake la mawaziri k...
Rais Ahmed Silanyo wa mkoa wa Somaliland alikutana na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Ulaya kwa Som...
(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji