Somaliland yawashitaki maafisa wa serikali waliotuhumiwa kwa wizi wa chakula cha msaada

Na Barkhad Dahir, Hargeisa

Aprili 18, 2012

  • 4 Maoni
  • Chapisha
  • Panga upya Punguza Ongeza

Maafisa watano wa serikali wamefikishwa mbele ya mahakama ya mkoa ya Hargeisa hapo Jumatatu (tarehe 16 Aprili) wakikabiliwa na mashitaka ya ubadhirifu wa chakula cha msaada.

  • Chumba cha Mahakama ya Hargeisa kilijaza watu zaidi ya uwezo wake katika siku ya mwanzo ya kesi, na kuwalazimisha wananchi waliokuwa wakifuatilia kesi kukusanyika nje. [Barkhad Dahir/Sabahi]

    Chumba cha Mahakama ya Hargeisa kilijaza watu zaidi ya uwezo wake katika siku ya mwanzo ya kesi, na kuwalazimisha wananchi waliokuwa wakifuatilia kesi kukusanyika nje. [Barkhad Dahir/Sabahi]

Washitakiwa hao wakiwemo mkurugenzi mkuu wa zamani wa Wizara ya Makaazi, Ahmed Elmi Bare; gavana wa zamani wa Maroodi Jeeh, Ahmed Omar Haji Abdullahi, na mshauri wa zamani wa Makamo wa Rais Abdirahman Abdullahi Ismail, Osman Said Jama.

Watu hao, waliokana mashitaka dhidi yao, walikamatwa tarehe 10 Machi baada ya kuondolewa rasmi kwenye nyadhifa zao kwa tamko la Rais wa Somaliland, Ahmed Mohamed Silanyo.

"Rais wa Jamhuri ya Somaliland ameamua kuwavua dhamana zao maafisa watatu baada ya kuridhika kwamba walihusika na ubadhirifu wa chakula cha msaada,” alisema msemaji wa serikali, Abdullahi Mohamed Dahir, katika taarifa ya mwezi uliopita.

Mkuu wa Jumuiya ya Ustawi wa Jamii ya Somaliland, Ahmed Ali Guled, aliyekuwa na dhamana ya kugawanya msaada wa chakula, na Abdishakur Abdi Nur, ambaye ni mmiliki wa ghala la vifaa vya ujenzi mjini Hargeisa, nao pia walikamatwa na sasa wanakabiliwa na mashitaka.

Wakili Mohamoud Abdirahman Nur, mmoja wa wanasheria wanaowawakilisha washukiwa, alisema watuhumiwa hao wanashutumiwa kwa kuchukua magunia 2,500 ya mchele na makatoni 400 za maharage.

Chakula hicho kilikuwa ni sehemu ya mzigo wa tani 100 ya msaada uliotolewa na Oman ambayo pia ilijumuisha nguo. Watu hao wanashukiwa kuipeleka shehena ya chakula kwenye ghala la mtu binafsi kwa ajili ya kugawiwa kwa matumizi binafsi, alisema Nur.

Watuhumiwa hao watano, waliojitokeza mahakamani Jumatatu, ni miongoni mwa watu 13 wanaotuhumiwa kuhusika katika kesi hiyo, walisema maafisa wa serikali.

“Watuhumiwa ambao kwa kiasi kikubwa wanatafutwa na vikosi vya usalama na yeyote aliyeshiriki kwenye mkasa huu, hata awe nani, atafikishwa mbele ya mahakama ya sheria,” alisema Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, Hassan Ahmed Aden, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hapo Jumatatu.

Aden alisema kwamba sheria inaagiza kesi kama hizi kufunguliwa ndani ya siku 45 tangu kukamatwa kwa watuhumiwa, na watuhumiwa hao wamekuwa kizuizini kwa mwezi mmoja tu. “[Wao] hawajawekwa kizuizini zaidi ya vile inavyotakiwa na sheria…haki zao hazijavunjwa,” alisema.

Abdihakim Mohamoud Shirwa, mwandishi wa habari aliyekuwepo mahakamani wakati kesi hiyo ikitajwa kwa mara ya mwanzo, aliiambia Sabahi kwamba kesi hiyo ilivutia watu wengi kwa sababu imekuwa ni mfano.

“Hii ni kesi ya kwanza ya aina yake,” alisema. “Ni mara ya kwanza kwa maafisa wa ngazi za juu serikalini wanaotuhumiwa kwa ufisadi kufutwa kazi, kukamatwa na kufikishwa mbele ya mahakama kwa historia ya Somaliland.”

Siku ya Jumatatu ni mashahidi watatu kati ya 28 wa upande wa serikali waliotoa ushahidi wao mahakamani, alisema Nur. Aliiambia Sabahi kwamba kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 21 Aprili.

“Natarajia haki itatendeka,” alisema.

Unaonaje kuhusu makala hii? (Jumla ya Kura 10)

Dislike_icon(0)

(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji

Maoni ya msomaji

  • Hussein Egal
    April 23, 2012 @ 08:36:13AM

    Ni jambo zuri kuzuwia ufisadi na watu wa Somaliland wamefurahi kweli kweli kusikia habari nzuri kama hiyo. Ningependa kuipongeza serikali kwa uamuzi mzuri iliochukua kupambana na ufisadi nchini.

  • Sada Nmirau
    April 22, 2012 @ 01:29:09PM

    Kama Waafrika, tunaithamini sana habari hii. Ufisadi ni ugonjwa wa kuambukiza ulioenea Afrika yote, hongera serikali ya Somalia katika kesi hii dhidi ya maafisa.

  • Mohamed Nur
    April 20, 2012 @ 06:45:02AM

    Hatimaye, wale waliokuwa hawagusiki wameguswa. Wanaojifaidisha kutokana na masikini wanastahiki adhabu kali. Hata hivyo, natumai kuwa kesi haitatumika kupindisha kukua kwa kukosa kukubalika kwa Silanyo na mabadiliko yake ya mawaziri ya kila mara. Ikiwa ni kweli, hivyo waendelee na kuleta haki, utawala uliopita wa Raisi Rayale na maafisa wake mafisadi ambao kwa mujibu wa Wizara ya fedha, waliiba dola za Kimarekani milioni 27 kutoka hazina ya serikali masikini.

  • Daadirow
    April 20, 2012 @ 12:47:45AM

    Jihadharini na ufisadi kwa sababu huharibu kila kitu katika nchi. Sioni nchi yoyote iliyoendelea inayoteseka kwa ufisadi, na sioni nchi yoyote ya dunia ya tatu ambayo haiteseki kutokana na ufisadi wa kifedha na wa kiuongozi. Kwa hivyo natumai serikali itatoa adhabu kali sana kwa wale watakaohusika na kesi za ufisadi wa kifedha au kiutawala. Walaaniwe, inakuwaje wanaiba chakula cha watu masikini?

Habari Mpya kabisa

Katika Mwangaza

Jisajili

Kura

Je, unadhania kupigwa marufuku kwa hotuba ya chuki na Tanzania kutakomesha mashambulizi dhidi ya makanisa na misikiti?

Angalia matokeo

Nyenzo