Serikali ya Somalia yatoa elimu, ajira kwa waasi wa al-Shabaab

Na Mahmoud Mohamed, Mogadishu

Machi 29, 2012

  • 3 Maoni
  • Chapisha
  • Panga upya Punguza Ongeza

Mpango wa kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida waasi wa al-Shabaab unawapatia wapiganaji wa zamani elimu na fursa za uajiri na ahadi za “hatima nzuri”, maafisa wa Serikali ya Mpito ya Shirikisho ya Somalia (TFG) na wanachama wa zamani wa al-Shabaab waliiambia Sabahi.

  • Washukiwa wapiganaji wanne wa al-Shabaab wakioneshwa hapo tarehe 22 Machi baada ya kukamatwa na vikosi vya Serikali ya Somalia na vya Umoja wa Afrika. Serikali inatoa msamaha na kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida waasi wa al-Shabaab. [Na Stuart Price/AFP]

    Washukiwa wapiganaji wanne wa al-Shabaab wakioneshwa hapo tarehe 22 Machi baada ya kukamatwa na vikosi vya Serikali ya Somalia na vya Umoja wa Afrika. Serikali inatoa msamaha na kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida waasi wa al-Shabaab. [Na Stuart Price/AFP]

Siku tatu baada ya TFG kutangaza ushindi dhidi ya al-Shabaab huko Mogadishu mwezi wa Agosti iliyopita, wakati kikundi cha wanamgambo kilipoondoka kwenye kambi zake mjini, serikali ilitangaza kuwa wapiganaji watakaoachana na kikundi cha wanamgambo watasamehewa.

Hivi karibuni, maafisa wa serikali za mitaa wametanua ahadi ya msamaha kwa waasi wa al-Shabaab katika maeneo mengine, hasa vijana.

“Serikali inawakaribisha waasi wa al-Shabaab, kuwasamehe na kuwapatia msaada kamili wa ustawi,” Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa wa Somalia Abdi Ali Hassan aliiambia Sabahi.

"Serikali ya Somalia kwa kushirikiana na marafiki zake wa jumuiya ya kimataifa – hasa Ofisi ya Kisiasa ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Mamlaka ya Baina ya Serikali kwa maendeleo, AMISOM na jumuiya nyingine – iko katika harakati za kuanzisha mpango unaokusudiwa kutoa elimu bila ya malipo na fursa za kazi kwa vijana walioasi kutoka al-Shabaab ili kuwawezesha kiakili na kiuchumi,” Hassan alisema.

“Serikali ya Somalia inaiomba jumuiya ya kimataifa kuisaidia mipango hii inayokusudia kutoa huduma za kuwawezesha kuisi maisha ya kawaida watoto hawa walioathiriwa na mzozo wa kivita, hasa wale waliopotoshwa na al-Shabaab,” alisema.

“Kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida waasi wa al-Shabaab 'kunaendelea vizuri'

Omar Ali Roble, waziri wa zamani wa upunguzaji wa silaha za kivita na kufungamana upya kwa wanamgambo, na kusisitiza umuhimu wa kutoa huduma zinazofaa za kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida kwa wapiganaji wa zamani wa al-Shabaab.

“Serikali imefanya uwawezeshaji wa kuisi maisha ya kawaida kwa waasi wa al-Shabaab ni suala la kipaumbele,” aliiambia Sabahi. “Wanatakiwa wapatiwe ushauri nasaha na itikadi tofauti na zile za kutiwa kasumba za al-Shabaab, na baadaye kuwapatia fursa kama vile huduma za elimu bila ya malipo na stadi nyingine muhimu za maisha ili waweze kujiendesha wenyewe – vinginevyo, wapiganaji hawa walioasi kutoka al-Shabaab wanaweza kuwa tishio kwa usalama.”

“Serikali lazima itumie fursa zilizopo kama vile msaada uliopo tayari kutoka jumuiya ya kimataifa ya kusaidia katika shughuli za kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida kwa waasi wa al-Shabaab,” Roble alisema. “Waasi hawa lazima wadhibitiwe mara moja, vinginevyo wanaweza kuwa kikwazo kwa usalama uliokwishapatikana nchini.”

Hassan alisema mpango huu wa kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida unashughulikia masuala haya.

“Mpango wa kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida waasi wa al-Shabaab unaendelea vyema,” alisema. “Wengine wamepatiwa huduma za elimu bila ya malipo. Wengine wanapewa mafunzo ya kuwapatia stadi muhimu ambapo baadaye watapatiwa kazi za kuboresha maisha yao huko mbele.”

Tangu serikali ilipotangaza mpango wake wa msamaha, idadi ya waasi ambao ama walijisalimisha kwa TFG au waliasi visivyo rasmi, imekuwa ikiongezeka kama kawaida.

Zaidi ya vijana 500 ambao waliasi kutoka al-Shabaab na kujisalimisha wenyewe kwa serikali tangu mpango wa msamaha ulipoanza, kwa mujibu wa msemaji mkuu wa serikali Abdirahman Omar Osman "Yariisow".

Osman alisema wapiganaji wa zamani wanawekwa katika vituo maalumu vya kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida kwa ajili ya waasi wa al-Shabaab.

Waasi wa al-Shabaab wawahimiza vijana wengine kujisalimisha

Sabahi ilizungumza na baadhi ya vijana ambao sasa wanaishi katika Kituo cha Mariino cha Waasi wa al-Shabaab.

Ali Hasan Elmi, mwenye umri wa miaka 24, alisema alikuwa mwanachama wa al-Shabaab kwa muda mrefu, lakini aliasi miezi kadhaa iliyopita.

“Tulipokelewa na vikosi vya TFG baada ya kujisalimisha na kila mmoja wetu alipewa dola za kimarekani 500 kwa silaha zetu,” aliiambia Sabahi. “Tulipelekwa mahali pazuri pa kuishi na tuliambiwa kuwa tutapatiwa elimu bila ya malipo. Pia tuliambiwa kuwa yeyote anayetaka ajira atapatiwa mafunzo maalumu yatakayotuwezesha kupata stadi muhimu na wale watakaoamua kujiunga na vikosi vya TFG watasaidiwa na serikali.”

Elmi alisema maisha yake yameimarika sana baada ya kuasi kutoka al-Shabaab na anapata msaada wa serikali.

“Ninapenda kuwataka vijana ambao bado wako na al-Shabaab kuhama huko na kujisalimisha wenyewe kwa TFG. Maisha yao yataimarika na watakuwa na hatima nzuri ikiwa wataondoka al-Shabaab,” Elmi alisema.

Abdirahman Mahamed Hashi, mwenye umri wa miaka 22, mpiganaji wa zamani wa al-Shabaab, aliiambia Sabahi, “Nimefurahi kuwa nilijisalimisha kwa serikali na kuondoka kwa al-Shabaab.”

“Tumesamehewa na serikali, tulitumia fursa hiyo na ninawataka wale vijana ambao bado wanapigana kwa ajili ya al-Shabaab kuasi kutoka kwao kama mimi,” alisema. “Wanamgambo hawaangalii masilahi yenu, bali wanataka muuliwe katika uwanja wa vita.”

Hashi alisema vijana waliaasi kutoka al-Shabaab wamefanya jukumu kubwa la kuvisaidia vikosi vya TFG kutuliza usalama nchini.

"Kuanzia wakati tulipojisalimisha kwa serikali, tulivisaidia vikosi katika kuwakamata wanachama kadhaa wa wanamgambo ambao walikuwa wanaishi na kujificha katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali,” alisema.

Mahamed Sheikh Ibrahim, afisa usalama wa zamani katika utawala wa Muungano wa Mahakama za Kiislamu, alisema vijana wengi wameiacha al-Shabaab katika miezi ya karibuni kwa sababu ya matatizo ya kifedha inaowakabili wanamgambo. Alisema wapiganaji wanapoteza matumaini ndani ya al-Shabaab na wanaugeukia msamaha wa serikali.

“Kwa baadhi ya sababu zinazohusiana na mgogoro baina ya viongozi wa al-Shabaab, matatizo ya kifedha ya wanamgambo na upungufu wa vifaa vya kijeshi, vijana wanaasi al-Shabaab na wanajisalimisha kwa serikali,” Ibrahim aliambia Sabahi. “Serikali imefanya jambo muhimu kwa kuwapokea wapiganaji walioasi na kuwahakikishia msamaha.”

Wawakilishi kutoka TFG, AMISOM, Mamlaka Baina ya Serikali kwa ajili ya Maendeleo, Ofisi ya Kisiasa ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia, pamoja na wabunge na wanaharakati wa asasi za kijamii walikutana katika mkutano wa siku mbili mjini Mogadishu hapo tarehe 17 na 18 Machi ili kubadilishana uzoefu wao katika kuandaa sera za namna gani kushughulikia kutojishirikisha, kuwachunguza na kuwafungamanisha upya wapiganaji wa zamani.

Unaonaje kuhusu makala hii? (Jumla ya Kura 12)

Dislike_icon(2)

(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji

Maoni ya msomaji

  • fanuel
    March 31, 2012 @ 11:43:24PM

    nakala hii imeandikwa kwa ufasaha sawia na ile ya kingereza,kiswahili sanifu na cha kueleweka.

  • Ramadhan
    March 31, 2012 @ 02:41:17AM

    yote haya yanasababiswa na ukosefu wa ajira

  • Msemaovyo
    March 30, 2012 @ 09:37:09AM

    Hili ni wazo zuri, lakini kama alivyoonya Omar Ali Roble na hapa ninamnukuu, “Wanatakiwa wapatiwe ushauri nasaha na itikadi tofauti na zile za kutiwa kasumba za al-Shabaab, na baadaye kuwapatia fursa kama vile huduma za elimu bila ya malipo na stadi nyingine muhimu za maisha ili waweze kujiendesha wenyewe...vinginevyo, wapiganaji hawa walioasi kutoka al-Shabaab wanaweza kuwa tishio kwa usalama,” kwa hivyo serikali na jumuiya za kimataifa lazima ziwe macho katika kulishughulikia suala hili. Ninatoa onyo juu ya hili kwa sababu tumezowea kuanzisha masuala nyeti kama hili lakini tunashindwa katika kuyaendeleza. Kuna sababu kadhaa za kushindwa kwa utekelezaji huo, lakini kubwa zaidi ni kuwa tunategemea sana wafadhili. Mara tu wafadhili wanapojitoa, miradi mizuri hubakia hewani. Sababu nyingine ni ufisadi. Wale waliopewa dhamana hutumia fedha za wafadhili kwa maslahi yao wenyewe badala ya kuzitumia kwa mradi uliopendekezwa. Mwisho lakini sio hayo tu, TFG lazima iwe na tahadhari katika kuwachunguza waasi ili kuepuka "kuwalea" al-Shabaab ambao wanaweza kujiingiza katika programu hii. Ninaitakia kila la heri programu hii ifanikiwe.

Habari Mpya kabisa

Katika Mwangaza

Jisajili

Kura

Je, serikali za majimbo ya shirikisho ziundwe vipi nchini Somalia kufuatia utata wa Jubbaland?

Angalia matokeo