Mgomo wa madaktari Tanzania uliwaumiza maelfu ya wagonjwa

Na Deodatus Balile, Dar es Salaam

Machi 15, 2012

  • 3 Maoni
  • Chapisha
  • Panga upya Punguza Ongeza

Maelfu ya wagonjwa waliathiriwa na mgomo wa madaktari nchini Tanzania, ambao ulisitishwa wiki iliyopita baada ya siku nne za mkwamo baina yao na serikali, kwa mujibu wa maafisa wa hospitali.

  • Mama kijana akisubiri kupata matibabu katika hospitali ya Temeke, Dar es Salaam mwaka 2007. Hivi sasa hospitali hiyo inapokea zaidi ya wagonjwa 2,000 kwa siku. [Roberto Schmidt/AFP]

    Mama kijana akisubiri kupata matibabu katika hospitali ya Temeke, Dar es Salaam mwaka 2007. Hivi sasa hospitali hiyo inapokea zaidi ya wagonjwa 2,000 kwa siku. [Roberto Schmidt/AFP]

Mgomo wa madaktari katika hospitali za umma ulipelekea idadi kubwa zaidi isiyo ya kawaida ya wagonjwa kuelekea katika hospitali kubwa za serikali kwa matibabu.

Afisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha, aliiambia Sabahi kwamba wagonjwa 2,700 waliathirika katika hospitali hiyo.

Muhimbili ndiyo hospitali kubwa kabisa nchini Tanzania na kwa wagonjwa kutoka nchini kote wanaohitaji huduma maalum, alisema Aligaesha.

Madaktari wote 259 wa hospitali walishiriki katika mgomo, na waaguzi 1,010 ambao walisema wasingeliweza kufanya kazi bila ya madaktari.

Kama hatua ya dharura, madaktari wakuu 67 wanaofanya kazi kwenye makao makuu ya Wizara ya Afya walipelekwa katika hospitali za jijini Dar es Salaam, na mipango ilikuwa ikifanywa ya kuwapeleka katika hospitali binafsi wale wagonjwa waliofurika kwenye hospitali za umma, kwa mujibu wa kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya Muhimbili, Dk. Donnan Mmbando.

Mganga mkuu wa hosptali ya Temeke, Dk. Amani Malima, alisema wagonjwa 10,000 waliathiriwa na mgomo huo wa nchi nzima.

“Fikiria hapa Temeke, idadi ya wagonjwa iliongezeka kutoka kiasi ya 1,500 kwa siku hadi zaidi ya 2,000. Tulikuwa hatuwezi kuihimili idadi hiyo, na hali ilikuwa hivyohivyo kwa hospitali nyingi,” Malima aliliambia gazeti linalomilikiwa na serikali la Habari Leo hapo Jumanne (tarehe 13 Machi).

“Hali ilikuwa mbaya,” alisema Aligaesha. “Tunamshukuru rais kwa kuingilia katikati wakati ambapo hali ilikuwa haidhibitiki tena.”

Wagonjwa waliachwa patupu

Mwalimu Adelina Porokwa mwenye umri wa miaka 46, wa jijini Dar es Salaam alisema alipaswa kusubiri siku tano nzima kwa madaktari kurudi kuja kumfanyia upasuaji uliopangwa kwa mtoto wake wa kike mwenye miaka 11, Annet. “Matayarisho yote yalikuwa tayari. Tulikuwa hata tumeishasaini kwa ajili ya operesheni yake, lakini ghafla tukaambiwa hapana madaktari wa kuifanya,” alisema.

“Hatimaye leo wamemfanyia operesheni kwa mafanikio,” Porokwa aliiambia Sabahi siku ya Jumanne. “Namshukuru Mungu, lakini hata sitaki kufikiria aina ya mateso aliyoyapitia.”

Porokwa alisema familia yake isingeliweza kumpeleka mtoto wake nje ya nchi kupata matibabu na alikuwa akihofia kuwa huenda mtoto wake angelikufa ikiwa madaktari wasingelirudi kazini. “Nilishapoteza matumaini, lakini sasa najisikia vizuri. Mungu yuko upande wangu,” alisema.

Siku ya Jumamosi, Salum Haji, ambaye ana ugonjwa unaohusiana na uti wa mgongo, aliiambia Sabahi kwamba alishuhudia wagonjwa watano wakipoteza maisha bila ya kuhudumiwa, na miili yao ikabakia kwenye wadi muda mrefu zaidi kuliko kawaida.

“Hii inatisha na inaogofya….ni kinyume na maadili kwa viwango vyote,” Haji aliiambia Sabahi. Alisema lazima serikali ilimalize suala hili kabisa na kwa lote.

Madai ya madaktari

Madai ya madaktari wa sekta ya umma yanajumuisha kuongezewa mishahara, kuboreshwa kwa mazingira ya kazi na kuwepo kwa vifaa bora zaidi vya kuwahudumia wagonjwa. Walitaka mshahara wa madaktari wapya uongezwe kutoka shilingi 950,000 hadi milioni 3.5, na wapate fedha za ziada kwa ajili ya kufanya kazi kwenye mazingira magumu, posho ya makaazi na usafiri. Madaktari pia waliomba bima ya afya kwa wafanyakazi wote kupitia Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa.

“Ikiwa tutayafanyia hesabu madai yote haya, daktari mmoja mpya atakuwa anapata shilingi milioni 7.7 za Kitanzania kwa mwezi. Matokeo yake, madaktari bingwa watapata hadi shilingi milioni 17,” alisema Rais Jakaya Kikwete hapo Jumatatu, akielezea wasiwasi wake kuwa mishahara iliyodaiwa ilikuwa mikubwa sana kwa serikali kuweza kulipa.

Hata hivyo, madaktari walisimamisha mgomo wao siku ya Jumatatu baada ya majadiliano makali katika siku nne za mkwamo na serikali.

“Tulikuwa na majadiliano makini na mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kwa masaa tisa mfululizo,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Tanzania, Dk. Namala Mkopi katika taarifa yake. “Mazungumzo hayo yamekuwa na faida sana na tunaamini kwa kile alichotuahidi….kwa hivyo, kwa taarifa hii, tunawataka madaktari wote nchini kurudi kazini mara moja kutoka sasa.”

Mkopi alielezea matarajio yake kwamba rais atayatatua masuala yaliyopo. “Yeye ndiye rais wa nchi hii na tunaamini anakusudia kufanya kile tulichokubaliana,” Mkopi aliwaambia waandishi wa habari hapo Jumapili baada ya madaktari kurudi kazini.

Kikwete alifikia makubaliano ambayo yaliwarudisha madaktari hospitalini. Alisema makubaliano rasmi yatafanyika chini ya kamati inayoongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, lakini bado hajapanga tarehe ya mkutano.

Huu ulikuwa ni mgomo wa pili wa madaktari kwa mwaka huu, wa mwanzo ukiwa ule uliochukuwa siku 17 katika miezi ya Januari na Februari.

Unaonaje kuhusu makala hii? (Jumla ya Kura 5)

Dislike_icon(2)

(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji

Maoni ya msomaji

  • MOSOTI ALEX
    March 19, 2012 @ 09:43:12AM

    Hivi watu hawa hawajifunzi kutokana na kile kinachoikabili Kenya hivi sasa?

  • scolastica yegon
    March 18, 2012 @ 12:15:06PM

    Madaktari wawashughulikie wagonjwa wanaokufa kwa vile madai yanashughulikiwa.

  • Msemaovyo
    March 16, 2012 @ 04:43:26PM

    Serikali inaweza kujihisi mshindi katika vita hivi vya mvutano na madaktari na wauguzi, lakini nahofia kuwa hakiwezi kufanyika chochote ili kutatua suala hili, kama ambavyo masuala mengine mengi hayajatatuliwa. Kwa kadiri ninavyoelewa jinsi Watanzania wamekuwa wakionewa na viongozi wao wababe na wenye majivuno, hakuna kamati itakayoundwa. Ilikuwa ni sababu hii, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye hatua yake ya kwanza ya kutatua tatizo hili wakati mgomo ulipotokea, yeye alisema “waache madaktari wagome, tutatumia madaktari wetu wa kijeshi badala ya kukaa na kukubaliana nao." Lakini hili halimshangazi yeyote kwa sababu Watanzania tayari wameshazoea ahadi hewa. Ni mara ngapi rais na wafuasi wake wamekuwa wakitoa hadi za matatizo makubwa? Moja ya ahadi yake ambayo bado haijatimizwa ilikuwa ile ya “Maisha bora kwa kila Mranzania”, ahadi ambayo haikutekelezwa kabisa. Pia wameshaahidi tena na tena juu ya umeme, kiasi kwamba sasa imekuwa kama mduara – kukiwa na ukame, hakuna umeme kwa sababu hakuna maji, maji yakiwepo mengi ya kuweza kuzalisha umeme, mashine hazifanyikazi. Kitu pekee nilicho na hakika nacho kuendelea ni ufisadi. Masikini Tanzania. Watanzania masikini!

Habari Mpya kabisa

Katika Mwangaza

Jisajili

Kura

Je, unadhania kupigwa marufuku kwa hotuba ya chuki na Tanzania kutakomesha mashambulizi dhidi ya makanisa na misikiti?

Angalia matokeo