Machi 02, 2012
Mwezi Oktoba 2011, Abdi Sulub Hussein aliwasili kwenye kambi ya wakimbizi ya Dadaab, akikimbia migogoro na ukame nchini Somalia, akitarajia kupata msaada atakapowasili.
Badala yake, yeye na maelfu ya wengine wakajikuta wakikabiliwa na vikwazo vya usalama vilivyochochewa na mashambulizi ya al-Shabaab na kuikwamisha utoaji wa misaada.
Utekwaji nyara wa madaktari watatu wa Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka hapo mwaka jana pamoja na kuuawa kwa maafisa kadhaa wa usalama wa Kenya na viongozi wawili wa wakimbizi kumeyaweka wazi matatizo wanayokabiliana nayo wakimbizi na wafanyakazi wa misaada makambini.
Mashambulizi haya yalileta wasiwasi miongoni mwa wafanyakazi wa misaada na mara moja baadhi ya mashirika ya kibinadamu yakajiondoa kwenye makambi hayo.
"Mke wangu na watoto wangu wanne hawajapokea msaada wowote wa kijamii tangu tulipokuja hapa tarehe 31 Oktoba,” Hussein aliiambia Sabahi. "Watoto wangu ni wagonjwa na wana njaa na tunategemea misaada ya wasamaria wema tu.”
Dadaab ni makazi ya mamia kwa maelfu ya wakimbizi na mara kwa mara huelezewa kama kambi kubwa kabisa ya wakimbizi duniani. Ikiwa ipo kwenye mpaka wa Somalia na Kenya, eneo hilo lina kambi tatu za wakimbizi: Ifo, Dagahaley na Hagadera. Mwanzoni ilikusudiwa iwe na wakimbizi 90,000 tu lakini sasa ina zaidi ya wakimbizi 463,000 wa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
Msemaji wa UNHCR nchini Kenya, Emmanuel Nyabera, alisema kumiminika kwa wakimbizi kumeongeza tatizo la ziada katika rasilimali zilizopo. Alisema Shirika la MSF, Jumuiya ya Misaada ya Kimataifa ya Ujerumani na Kamati ya Uokozi ya Kimataifa ziliondosha wafanyakazi wake kwenye kambi za Dadaab.
Sabahi ilifanya mahojiano na wafanyakazi wa misaada, ambao walisema kuwa eneo la huduma za afya limeathirika vibaya na kuondoka kwa mashirika hayo.
"Shirika la Msalaba Mwekundu lilichukuwa nafasi baada ya MSF (Madaktari Wasio na Mipaka) kuondoka, lakini kadiri wanavyojitahidi, hawawezi kukidhi mahitaji makubwa ya huduma za afya yaliyopo,” alisema Moulid Abdi, mfanyakazi aliyejitolea kufanya kazi na mashirika ya misaada.
"Watu wanateseka,” aliiambia Sabahi. "Tangu MSF waondoke, nafasi yao haijajazwa.”
“Sio tu afya. Eneo la maji pia limeathirika. Si kama ilivyokuwa mwanzoni,” alisema Abdi, akiongeza kwamba wafanyakazi wa misaada wa kigeni hawatembei tena kwa uhuru kwenye makambi kama walivyokuwa wakifanya. “Wamo maofisini mwao tu, wachache ndo hutoka nje kidogo wakihofia usalama wao, na hata wakitoka nje hawaendi mbali,” alisema.
Nyabera alisema timu za UNHCR zimekuwa zikishiriki katika ulinzi na kazi za huduma kwa jamii.
“Mapema mwezi Februari, UNHCR ilihamishia makazi ya wakimbizi kutoka yale yenye usalama mdogo katika kambi ya Dagahaley kwenda kwenye kambi mpya ya Ifo II, ambako walipokea mahema kwa ajili ya familia, mahitaji na huduma za msingi. Kiasi ya wakimbizi 2,000 wameshahamishiwa huko hadi sasa, huku wengine 3,500 wakipangiwa kupelekwa huko wiki zijazo. Hadi mwisho wa zoezi hilo, kambi nzima ya Ifo II yenye nafasi ya kuchukuwa wakimbizi 80,000 itakuwa imejaa,” alisema. Kambi ya Ifo II ilifunguliwa Julai 2011 ili kupunguza mrundikano kwenye kambi za Dadaab.
Serikali ya Kenya inasema kwamba imeongeza ulinzi katika makambi ili kuhakikisha kuwa wakimbizi wanapata huduma kama kawaida.
Mkuu wa Wilaya ya Dadaab, Bernard ole Kipury, aliiambia Sabahi kwamba kwa miezi mitatu iliyopita hakujakuwa na wakimbizi wapya. “Hata hivyo, tumeimarisha hatua za kiusalama, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa taarifa za kijasusi, kuhakikisha zinafanyiwa kazi vyema,” alisema.
"Vilevile tumeyashauri mashirika ya kibinadamu yanayofanya kazi kwenye makambi kushirikiana nasi kuratibu usalama wao,” alisema akiongeza kwamba baadhi ya wafanyakazi wa misaada waliokuwa wameacha kutoa huduma, sasa wameanza kurudi.
Kipury pia alisema kwamba miminiko wa wakimbizi kwenye makambi umepungua kwa sababu ya operesheni ya vikosi vya Kenya na pia mvua inayoripotiwa kunyesha nchini Somalia.
"Wakimbizi wengi walikuja Kenya kwa sababu ya ukame na sio vita. Baada ya mvua za mwezi Oktoba, wengi waliondoka na kambi mpya ya Ifo II ina wakimbizi wengi zaidi kuliko nyingine tatu za Dagahaley, Ifo na Hagaldera," alisema.
Nyabera alisema kwamba mashirika yaliyoondowa wafanyakazi wake sasa yanahakiki hali ya mambo na yanatarajiwa kurudisha huduma zao za kawaida. Alisema huduma za kunusuru maisha kama vile msaada wa chakula, maji na afya zinaendelea.
Msemaji wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa nchini Kenya, Rose Ogola, alisema waliondoa wafanyakazi wao kutoka Mandera kwa sababu ya ukosefu wa usalama, lakini wafanyakzi katika kambi za Dadaab bado walisilia.
“Wafanyakazi wetu wa Dadaab bado wako licha ya changamoto za usalama. Usalama wa wafanyakazi wetu ni jambo la kwanza, lakini wakati huohuo huduma kwa wakimbizi pia zina umuhimu huohuo,” Ogola aliiambia Sabahi.
"Watoaji huduma za kibinadamu wameangalia njia mbalimbali za kurudisha shughuli zao, kwa kutumia mbinu tofauti, ikiwemo ya kukabidhi majukumu zaidi kwa jamii za wakimbizi,” alisema Nyabera. “Shule zinaendeshwa kwa kiasi kikubwa na walimu wakimbizi zimefungua na ziliweza kufanya mitihani ya taifa ya Kenya mwishoni mwa mwaka 2011 licha ya kuzorota wa usalama,” alisema.
"Mgogoro huu ulitoa fursa ya kuwawezesha wakimbizi kushughulikia mambo ya kila siku ya kimaisha kwenye kambi,” Nyabera alisema. “Mabadiliko yalijumuisha kuwashirikisha vijana katika kuwapatia wakimbizi wapya elimu, kuratibu kamati za maji na kuhakikisha maji ya kutosha kwa kila nyumba, waandishi wa habari wakimbizi wakichapisha gazeti lao wenyewe, na wanawake kuunda makundi ya kuimarisha maisha kwa akina mama,” alisema.
Nyabera alisema huduma zimekuwa zikiimarika, lakini bado kumekuwepo na mlipuko wa maradhi. “Bado tunashuhudia maambukizi mapya za surua, 11 katika wiki iliyopita, na sasa tunajikita katika kuwapa chanjo wakimbizi wote wapya walio kwenye umri wa miaka 30 na kuendelea,” alisema.
Balozi wa Somalia nchini Kenya, Mohamed Ali Noor, aliiambia Sabahi kuwa shirika la MSF limeahidi kurudisha huduma zake makambini.
“Kuna mahitaji makubwa ya MSF kwa makundi yaliyo hatarini kama vile watoto na wanawake. Wale wanaowasili makambini huwa wametembea kwa masafa marefu, lakini hawakuti mtu wa kuwahudumia. Ninajuwa kuhusu kuwepo kwa wakimbizi wapya ambao hawajasajiliwa kwa sababu ya michakato mirefu,” alisema.
"Hata hivyo, nimezungumza na MSF na wameniambia kuwa wanafikiria kuwapeleka wafanyakazi wao kwenye kambi za Dadaab,” alisema. “Waliniambia wanatiwa wasiwasi na hali ya usalama, lakini serikali ya Kenya imeahidi kuimarisha usalama.” b
"Vilevile nimewaomba Wasomalia wanoishi nchini Kenya kufanya kazi na serikali kufichua dalili mbaya zinazosababisha fujo. Wanapaswa kuheshimu sheria za mwenyeji wao kuimarisha mahusiano mema na kujua kwamba al-Shabaab ni kitisho,” Noor alisema.
Wakati huohuo, Noor alisema kuwa Wasomali kadhaa wanaoishi nje wamejitolea kutoa huduma muhimu kwenye makambi.
“Kutakuwa na makundi yatakayojitolea kila mwisho wa wiki na mengine yatakayokwenda huko kila mwezi,” alisema. Pamoja na hayo ubalozi wa Kuwait nchini Kenya utatuma ujumbe wa wataalamu wa afya katika hospitali za Dadaab ili kusaidia operesheni, alisema Noor.
Wizara ya Usafiri wa Anga ya mkoa wa Somaliland siku ya Jumanne (tarehe 18 Juni) iliikataza ndege...
Polisi nchini Tanzania waliwakamata makamu wanne wa chama kikuu cha upinzani cha Demokrasia na Ma...
Watu wenye silaha kwenye Kaunti ya Wajir walimuua polisi mmoja wa akiba wa Kenya siku ya Jumanne ...
Japan inaipa Tanzania dola milioni 49 (shilingi bilioni 80.4) kama msaada na mkopo kwa ajili ya k...
Inspekta Jenerali wa Polisi David Kimaiyo yeye pekee yake amewateua na kuwapangia kazi maafisa wa...
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) siku ya Jumanne ilimkubalia Makamu wa Rais wa Kenya Willia...
Polisi waliwakamata mamia ya watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa al-Shabaab katika wilaya za Hod...
Kongamano la siku tatu juu ya elimu lilifunguliwa mjini Mogadishu siku ya Jumanne (tarehe 18 Juni...
Wanajeshi wa serikali ya Somalia wakisaidiwa na wanajeshi wa Misheni wa Umoja wa Mataifa (AMISOM)...
Waziri wa Mambo ya Ndani na Uratibu wa Serikali ya Kitaifa, Joseph Ole Lenku, siku ya Jumatatu (t...
(Sera za kutoa Maoni) *Inaonesha Maeneo yanayohitaji
Maoni ya msomaji
Somalia inajulikana kama mojawapo ya nchi masikini kabisa ulimwenguni. Idadi kubwa ya watu hawana ajira na wanaishi katika hali mbaya sana ya umasikini. Watu hawana chochote cha kula na hawana maji ya kutosha ya kunywa. Hawana pahali pa kujihifadhi. Chakula na maji ambavyo ni muhimu sana kwa maisha ya binadammu, havipatikani kule na kwa sababu ya mambo haya, idadi kubwa ya watu wanaathirika na hali ya uutapiamlo. Pamoja na mashaka haya, wanamgambo wa kikundi cha kigaidi cha al-Shabaab ambao vilevile wanalenga watu masikini wa Somalia ili kupata muda zaidi na kuliteka taifa la Somalia ili waweze kuendesa vitendo vya kigaidi. Al-Shabaab ni sehemu ya al-Qaeda ambao pia walihusika na mlipuko wa tarehe 11 Septemba huko Marekani.
Jukumu kubwa la shirika la kibinadamu ni kusaidia watu ambao hawapati mahitaji yao ya msingi kama vile chakula, maji n.k. Na taifa la Somalia ni moja katika ya mataifa masikini sana ulimwenguni kote. Watu kule hawana chochote cha kula na kunywa. Hawana pahali pa kujisitiri wenyewe. Kuna vitu vingi kule vinavyochangia mashirika ya kibinadamu kutokuwa na uwezo wa kuwasaidia watu nchi Somalia, lakini sababu kubwa ni kikundi cha wanamgambo wa al-Shabaab ambao wako Somalia ili kueneza hisia za kuwepo ugaidi.
Hali duni ya uchumi katika nchi kama Somalia husababishwa na ukosefu wa amani na uthabiti. Tuhuma baina ya makundi tofauti, yaani mashirika ya magaidi na wanamgambo wa koo fulani, zinazorotesha hali ya uthabiti. Ijapokuwa walinda amani wa Umoja wa Afrika wanafanya ari kuleta amani na uwiano, wanakundi wa mashirika yenye siasa kali kama Al-Qaeda na Al-Shabaab hawako tayari kufuata njia ya mazungumzo na maafikiano, bali mwito wao ni kufuata sheria ya Kiislamu ya ‘Sharia’ kwa njia ya kikamilifu bila kukengeua. Pia wanadai kwamba sharti majeshi yote ya kigeni waondoke Somalia. Kwa hivyo, maoni yangu ni kwamba mazungumzo mazito zaidi yanayohusisha vikundi vingi vya kizalendo ndiyo yatakayoleta amani katika nchi hii maskini. Mpaka sasa majaribio ya Utume wa Umoja wa Afrika katika Somalia kuanzisha mazungumzo na hawa magaidi yameambulia patupu. Hivi juzi mawasiliano kwa njia ya mitandao na vyombo vya habari yamekaribishwa na wanamgambo hao kuelezea dunia nzima ajenda yao. Huenda mawasiliano haya yataanzisha mazungumzo baina ya magaidi wa Al-Shabaab na watu wengine duniani.
Umoja wa Mataifa daima umekuwa ukifanya kazi ngumu ya kuwasaidia watu. Somalia sio nchi pekee ambayo inapitia katika wakati mgumu. Kusema kweli, hivi sasa, watu wana maisha mazuri. Hii ni matokeo ya programu zinazoendeshwa na Umoja na Mataifa zinazoshughulikia maendeleo na ulinzi wa watu wa Somalia ambazo zimekuwa zikiendeshwa tangu miaka ya 90 wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza nchini Somalia. Umoja wa Mataifa siku zote umekuwa ukijaribu kutafuta ufumbuzi juu ya mzozo wa Somalia. Imekuwa ikipambana na kuwalisha raia ambao wamekwama katika vita baina ya vikundi vidogo vidogo vinavyopigana. Pia, Umoja wa Mataifa umejaribu kuwalinda wale waliokuwa hawapigani, kutoka hofu inayosababishwa na vikundi hivi. Kwa kufanya hivi, walipelekwa majeshi ya kulinda amani ambao wamekuwepo Somalia kwa miongo mingi sasa. Shughuli zao zinalenga katika kuwatetea raia dhidi ya mauji na hofu inayoletwa na wale wanaokaribisha na kuhamasisha mgogoro ndani ya jamii ya Somalia. Kwa kweli Umoja wa Mataifa unastahiki kuthaminiwa na kushukuriwa kwa kazi yake nchini Somalia kwa muda wote huu. Imeweza kuendelea na operesheni zake mpaka leo licha ya kuendelea kwa vurugu ambazo zinakwamisha kazi zake katika maeneo yanayoathiriwa na vita.
Kundi la Al-Shabaab, lenye wafuasi 14,426, linaweza kutambulishwa kama kundi la kigaidi, kundi la kimapinduzi ama nyendo. Wakidai kuwa wao ni kundi ia Uislamu la Jihad, hiki chama cha siasa kali kimezidi kueneza mafunzo haramu yasiyoambatana na kanuni za Uislamu (kwa mfano vurugu na ghasia). Aidha dini ya Uislamu inatitilia mkazo amani na upatanifu badala ya vurugu na utumiaji wa nguvu. Kusema kweli kundi kinachounga mkono siasa kali halifaidishi wananchi Wasomali, kwani matakwa yao haswa ni msaada na maridhiano yatakayowawezesha kutatua shida zao. Kundi la Al-Shabaab limehusika katika mashambulio ya kujitoa mhanga ambayo yameharibu miundo msingi ya takriban nusu ya nchi ya Somalia. Kwingine, ili kutimiza mahitaji yao, wanakundi wa Al-Shabaab wamedai mlungula kwa maharamia ili kuwalinda na kuwasetiri. Wanaharakati wa Al-Shabaab wanachukiwa kwa uadui wanaoonyesha masharika ya kiutu. Mara kwa mara, wanawateka na hata kuwaua hawa watu waliojitolea kuwasaidia Wasomali waliokumbwa na njaa.
Hakuna shaka ushawishi wa al-Shabaab utahatarisha na utakuwa na athari kubwa sana kwa maisha ya watu ikiwa hawakudhibitiwa. Ushawishi wao kwa sasa unasambaa kama moto katika kichaka kwa kila mtu anayeishi ndani na maeneo ya karibu. Kwa hivyo, vijana wengi wasio na ajira ambao kiafya wako imara na hawana kazi watajiunga na al-Shabaab ili waweze kujikimu na familia zao kwa sababu watakuwa wanalipwa vizuri ili kutekeleza vitendo vya kigaidi kwa kuwamaliza wale wanaopingana na itikadi zao. Hii itakuwa na athari ya kuimarisha uwepo wa vikundi vya kigaidi kama al-Shabaab na kueneza ujumbe wao wa vitisho nchini kote siku hadi siku. Serikali na mashirika ya misaada kwa hivyo lazima yafanye kazi mkono kwa mkono kuweka pamoja rasilimali na fedha ili kuanzisha programu za kuwawezesha vijana kiuchumi na kazi kwa ajili yao ili waweze kujikimu maisha yao na ya familia zao. Kwa njia hii, serikali na mashirika ya misaada yataweza kuwavutia vijana ambao kwa sasa wanakwenda kuiimarisha al-Shabaab ambao wanasababisha vurugu na vita katika nchi ambayo wanasababisha umwagaji damu zaidi, kujiunga na chuki zao na kuimarisha mtindo wao wa sharia.
Licha ya majaribio mengi ya Umoja wa Mataifa kuwasaidia wananchi wa Somalia, na licha ya vitendo bora vya kuangamiza baa la njaa, shughuli za vyama kutoa msaada na faraja hazikuleta matokeo yaliyotarajiwa. Wito wa Kiutu wa 2012 uliofanywa na Marekani utawanufaisha asilimia arobaini ya Wasomali. Nao watafaidika kwa kupokea vyeti vya bure, na pembejeo za dharura za ukulima na za uvuvi. Umoja wa Mataifa unakisi kwamba zaidi ya watu milioni kumi na tatu wanahitaji usaidizi wa dharura katika nchi za Uhabeshi, Kenya na Somalia. Kufuatia hali ya ukosefu wa usalama, makundi ya kiutu nchini Marekani yamesita katika utekelezaji wa miradi yao ya kusaidia Wasomali. Mvua kubwa iliyoanguka katika mwezi wa Novemba 2011 ilitatiza shughuli za kuwasilisha msaada kwa maeneo wenye mafukara. Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilikuwa na wasiwasi kuhusu uwezo wa kuwalipa fidia kimaadili wale Wasomali waliopoteza mali, kujeruhiwa au kupoteza maisha yao kutokana na shughuli za kivita na zinginezo. Hali ya hewa ndiyo iliyochangia zaidi katika kuvuruga shughuli za Umoja wa Mataifa za kutoa msaada.